Nov 22, 2023 06:38 UTC
  • Watu 37 wafariki dunia katika mkanyagano wa uandikishaji makuruta Congo Brazzaville

Vijana wapatao 37 wamefariki dunia kufuatia mkanyagano uliotokea wakati wa zoezi la kuwasajili makuruta wa kijeshi katika mji mkuu wa Jamhuri ya Congo ya Brazzaville.

Waziri Mkuu Anatole Collinet Makosso amethibitisha tukio hilo na kusema kuwa, idadi isiyojulikana ya watu wengine wamejeruhiwa.

"Kitengo cha mgogoro kimeanzishwa chini ya mamlaka ya waziri mkuu," taarifa iliongeza. Maelezo mengine kuhusu tukio hilo bado hayajaeleweka.

Watu waliotarajiwa kuajiriwa walikuwa wameelekezwa kwenda kwenye Uwanja wa Michel d'Ornano katikati mwa Brazzaville.

Kulingana na wakaazi wa eneo hilo, watu wengi walikuweko uwanjani Jumatatu usiku wakati mkanyagano ulipoanza. Baadhi ya watu walikuwa wamejaribu kuingia kwa nguvu kupitia lango kuu, huku wengi wakikanyagwa katika tukio hilo, mashuhuda wamesema.

Wiki iliyopita, jeshi katika taifa hilo la Afrika ya kati pia linalojulikana kama Congo-Brazzaville, lilitangaza kuwa linaajiri watu 1,500 wenye umri wa kati ya miaka 18 na 25.

Hadi sasa chanzo cha mkasa huo hakijabainika wazi, lakini mashuhuda wamesema baadhi ya watu walikuwa wakijaribu kuingia kwa nguvu uwanjani hapo, jambo lililosababisha mkanyakagano.

Ukosefu wa ajira umekithiri katika nchi hiyo yenye watu milioni 5.8, ambapo kulingana na Benki ya Dunia, "asilimia 75 ya wafanyakazi wa Kongo Brazzaville wameajiriwa katika sekta isiyo rasmi, ama ya kujiajiri au katika kazi zisizo na tija.