Nov 25, 2023 12:11 UTC
  • Abdelmadjid Tebboune
    Abdelmadjid Tebboune

Rais wa Algeria amesema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepatwa na maradhi ya kupooza na kwamba utawala ghasibu wa Israel haujali wala kuheshimu maamuzi ya taasisi hiyo ya kimataifa.

Katika hotuba yake kwenye mkutano wa 15 wa Kundi la 10 la Umoja wa Afrika, ambalo linafuatilia suala la mageuzi ndani ya Baraza la Usalama, Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune, amesema: Mkutano huu unafanyika katika kivuli cha kupooza kwa Baraza la Usalama la UN na katika kipindi ambapo mgogoro mkubwa umevuruga mfumo wa usalama.

Rais wa Jamhuri ya Algeria aidha ameeleza kuwa, hii leo Baraza la Usalama linashuhudia migogoro na mapigano mfululizo bila ya kuchukuliwa hatua za kweli na halisi au kubuni mpango madhubuti wa kisiasa.

Rais Abdelmadjid Tebboune ameongeza kuwa: "Wapalestina wanakabiliwa na janga halisi, ambalo linazidi kuwa baya siku hadi siku kutokana na udhaifu wa taasisi za Umoja wa Mataifa na jumuiya za kimataifa, na kukosa wa uwezo wa kuuzuia utawala ghasibu wa Israel kufanya jinai zake na kuacha kukiuka sheria za kimataifa."

Vilevile ameeleza kuwa, utawala wa Kizayuni hautilii maanani hata kidogo Umoja wa Mataifa na unapuuza yale yanayoidhinishwa na taasisi hiyo na kukiuka wajibu na majukumu yake.

Baraza la Usalama

Rais wa Jamhuri ya Algeria kwa mara nyingine amesisitiza udharura wa kusahihisha na kufidiwa dhulma zilizofanywa dhidi la bara la Afrika na kusema kuwa, licha ya kwamba bara hilo linahushwa na zaidi ya asilimia 70 ya masuala yaliyomo katika ajenda za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini ndilo pekee ambalo halina mwakilishi katika kundi la wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ni mara chache sana kuwa na wawakilishi kati ya wanachama wasio wa kudumu wa baraza hilo.

Tags