Apr 24, 2024 06:52 UTC
  • Jumatatu, 22 Aprili, 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 13 Mfunguo Mosi Shawwal 1445 Hijria sawa na tarehe 22 Aprili 2024.

Siku kama ya leo tarehe 3 mwezi Ordibehesht katika kalenda ya mwaka wa Kiirani ni siku ya kumuenzi Sheikh Bahauddin Muhammad Amili, maarufu kwa jina la Sheikh Bahai, mwanazoni mkubwa wa taaluma mbalimbali za Kiislamu. Sheikh Bahai ambaye alikuwa ametabahari katika elimu nyingi kama fiqhi, nujumu, Hadithi, tafsiri ya Qur'ani na hesabati alifariki dunia katika mji wa Isfahan nchini Iran. Alizaliwa mwaka 953 Hijria katika mji wa Baalabak huko Lebanon katika familia ya Kiirani. Baba yake alikuwa miongoni mwa mashekhe wakubwa wa zama hizo. Sheikh Bahai ameandika vitabu zaidi ya mia moja ikiwa ni pamoja na Tashrihul Aflak, Kashkul na Hablul Matin.

Sanamu la Sheikh Bahai

Siku kama ya leo miaka 300 iliyopita, alizaliwa Immanuel Kant, mwanafalsafa mkubwa wa Ujerumani katika eneo la Königsberg. Baada ya kuhitimu masomo katika taaluma ya hisabati, theolojia na falsafa Kant alijishughulisha na kazi ya ufundishaji vijijini. Baadaye msomi huyo alifanikiwa kuwa mhadhiri wa falsafa katika chuo kikuu cha mji alikozaliwa wa Königsberg.

Katika miaka yote ya utafiti wake na kufundisha falsafa, alipata kuandika vitabu tofauti ambavyo baadhi vipo katika maktaba kubwa duniani. Kadhalika mwanafalsafa huyo mkubwa alifanikiwa kuasisi mfumo wa kifikra maalumu katika uga huo.

Kwa imani ya Immanuel Kant, ndani ya mwanadamu kuna hisia maalumu ya kitabia ambayo huweza kutoa hukumu kwamba kitendo hiki ni chema na kile ni kiovu. Hii ikiwa na maana kwamba, mwanadamu binafasi anaweza kutenda mema na maovu, lakini ile hisia yake ya kitabia ndio huweza kumueleza kwamba kitendo fulani ni chema au kibaya na kwamba lau kama si kuwepo kwa hisia hiyo, basi mwanadamu asingeweza mwenyewe kujilaumu baada ya kutenda jambo fulani. 

Immanuel Kant alifariki dunia tarehe 12 Februari 1904 mjini Königsberg akiwa na umri wa miaka 80 huku akiwa ameishi maisha yake yote akiwa kapera.

Immanuel Kant

Siku kama hii ya leo miaka 129 iliyopita wananchi wa Cuba kwa mara nyingine tena walianzisha mapambano ya kupigania uhuru wao kutoka kwa wakoloni wa Uhispania.

Hayo yalikuwa mapambano yao ya tatu katika nusu ya pili ya karne ya 19 Miladia kwa ajili ya kutaka kujitawala. Uhispania ilituma wanajeshi laki tatu nchini humo kwa ajili ya kupambana na wanamapinduzi hao. Kufuatia vurugu hizo Marekani ilitumia fursa hiyo na kwa kisingizio cha kulipuliwa meli yake ya kivita karibu na pwani ya Cuba mwaka 1898 Miladia, kuingia katika vita hivyo dhidi ya Uhispania.

Manuwari za kivita za Uhispania ziliangamizwa katika maji ya Cuba na hatimaye nchi hiyo ya Amerika ya Latini ikakaliwa kwa mabavu na Marekani.

Bendera ya Cuba

Miaka 120 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa mwanafizikia na mtengenezaji wa bomu la atomiki wa Marekani Robert Oppenheimer.

Kabla ya Vita vya Pili vya Dunia mtaalamu huyo alifanya utafiti kuhusiana na jinsi ya kupasua atomu na kupata nishati ya nyuklia. Wakati wa vita hivyo alipewa wadhifa wa kusimamia kitengo cha utafiti katika Wizara ya Vita ya Marekani na chini ya usimamizi wake yakatengenezwa mabomu matatu ya kwanza ya nyuklia.

Hata hivyo, wakati Marekani ilipoishambulia Japan kwa mabomu ya nyuklia mwaka 1945, makumi ya maelfu ya watu wasio na hatia waliuawa katika kipindi kifupi, hali iliyomfanya Oppenheimer kujutia kitendo chake hicho na akatoa wito wa kutumiwa nishati ya atomiki katika masuala ya amani.

Robert Oppenheimer

Miaka 76 iliyopita mwafaka na siku kama hii ya leo, yaani tarehe 22 Aprili 1948, Wazayuni waliushambulia mji wa bandari wa Haifa huko kaskazini magharibi mwa Palestina wakati wa kukaribia kuanzishwa utawala haramu wa Israel.

Wazayuni waliwauwa shahidi Wapalestina 500 katika mashambulizi hayo makubwa na kuwajeruhi wengine 200 ambao walikuwa wanawake na watoto waliokimbilia huko Haifa wakisubiri kupelekwa katika maeneo mengine.

Tarehe 3 Ordibehest miaka 40 iliyopita utawala wa Kibaath wa Iraq ulianzisha vita na mashambulizi dhidi ya meli za kubeba mafuta za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika maji ya Ghuba ya Uajemi.

Baada ya kupita karibu miaka minne tangu Saddam Hussein aivamie ardhi ya Iran, Iraq ikisaidiwa na madola makubwa, ilichukua hatua ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya Iran kwa kutumia wenzo wa kuzuia uuzaji nje mafuta ya Iran na badala yake wazidishe uzalisha wa mafuta katika nchi za Kiarabu ili kufidia nakisi ya mafuta ya Iran katika masoko ya kimataifa. Kwa misingi huo walianza kushambulia meli za kubeba mafuta za Iran na bandari za kupakia bidhaa hiyo hapa nchini.

Siku hiyo Iraq ikisaidiwa na Marekani na nchi nyingine za Magharibi, ilitumia ndege za kivita za Super Standard za Ufaransa kushambulia kisiwa cha Khark na meli zilizokuwa zimebeba mafuta za Iran.

 

Tags