Nov 26, 2023 06:29 UTC
  • Rajoelina ashinda kiti cha urais Madagascar kwa muhula wa tatu

Tume ya Uchaguzi ya Madagascar jana Jumamosi ilitangaza kuwa Andry Rajoelina ameshinda tena kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wa tatu katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Rais uliosusiwa na karibu wagombea wote wa upinzani.

Tume hiyo imeeleza kuwa, Rajoelina ameshinda duru ya kwanza ya uchaguzi wa Rais kwa kupata asilimia 58.9 ya kura zilizopigwa. Akizungumza katika mji mkuu wa Madagascar, Antananarivo, Andry Rajoelina amewapongeza wananchi wa Madagascar kwa kumchagua tena kuliongoza taifa hilo linaloundwa na viisiwa vinavyopatikana katika Bahari ya Hindi. 

Ameongeza kuwa: "Katika uchaguzi wa rais mwaka huu nimepata kura zaidi ya milioni 2 na 850,000 jambo linalonyesha azma ya wananchi wa Madagascar ya kuendeleza njia ya maendeleo na ustawi wa nchi." 

Katika uchaguzi wa Rais wa Madagascar uliofanyika mwaka 2018, duru ya pili ilikuwa muhimu kwa Rajoelina kushinda kiti cha urais. Wakati huo Rajoelina alishinda  kwa kupata kura milioni 2 na 586,938.  

Muungano wa upinzani Madagascar umesema kuwa hautayatambua matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 16 mwezi huu ambapo Andrey Rajoelina ametangazwa mshindi. 

Tags