Mar 29, 2024 02:38 UTC
  • Kimbunga cha Gamane chaipiga Madagascar, 11 waaga dunia

Watu wasiopungua 11 wameaga dunia baada ya kimbunga kikali cha tropiki cha Gamane kuipiga Madagascar.

Hayo yalisemwa jana Alkhamisi na Jenerali Elack Andriakaja, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Kudhibiti Hatari na Majanga ya Madagascar (BNGRC) na kuongeza kuwa, mbali na watu 11 kuthibitishwa kuaga dunia kwenye janga hilo la kimaumbile, makumi ya wengine wametoweka, huku maelfu wakiathiriwa.

Amesema watu 7,000 wameathiriwa na kimbunga hicho katika wilaya ya Vohemar na wilaya nyingine kadhaa za kaskazini mwa kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi. Ofisi hiyo pia imesajili matukio kadhaa ya maporomo ya udongo. 

Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Kudhibiti Hatari na Majanga ya Madagascar pia imesema, maji yamefurika kwenye makumi ya nyumba huku nyumba nyingine kadhaa zikiharibiwa kabisa.

Athari za kimbunga Madagascar

Vimbunga vimekuwa vikiikumbwa Madagascar mara kwa mara, ambavyo husababisha maafa makubwa ya roho na mali. Malaki ya watu wamekuwa wakiacha bila makazi, huku miundombinu na mifumo ya mawasiliano ikiharibiwa vibaya.

Mwaka mmoja uliopita, watu zaidi ya 500 walipoteza maisha baada ya kimbunga cha Freddy kuipiga Madagascar na nchi jirani za Msumbiji na Malawi.

Aidha Januari mwaka jana, makumi ya watu waliaga dunia baada ya kimbunga cha tropiki cha Cheneso kupiga pwani ya kaskazini mashariki mwa kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi na kuelekea kusini-magharibi.

Tags