Feb 13, 2024 07:32 UTC
  • Sheria inayoruhusu kuwahasi wabakaji Madagascar yalalamikiwa na makundi ya kutetea haki

Bunge la Madagascar limepitisha sheria inayoruhusu kuwahasi kwa kemikali na katika baadhi ya kesi kwa njia ya upasuaji watu wanaopatikana na hatia ya kubaka watoto wadogo.

Hata hivyo, sheria hiyo imekabiliwa na ukosoaji wa makundi ya kimataifa ya kutetea haki lakini pia kuungwa mkono na wanaharakati ambao wanasema ni kinga mwafaka ya kuzuia kile kinachoelezwa kama "utamaduni wa ubakaji" uliozagaa nchini humo.
 
Bunge la Madagascar yenye idadi ya watu milioni 28 lilipitisha sheria hiyo mnamo Februari Pili na Baraza la Seneti, ambalo ni bunge la juu, liliiidhinisha wiki iliyopita. Sheria hiyo sasa inahitaji iidhinishwe na Mahakama Kuu ya Katiba na kutiwa saini kuwa sheria na Rais Andry Rajoelina, ambaye alizungumzia suala hilo kwa mara ya kwanza mwezi Desemba, sambamba na serikali yake kupendekeza mabadiliko ya sheria ya ubakaji.
 
Waziri wa Sheria Landy Mbolatiana Randriamanantenasoa amesema, kuwahasi wabakaji ni hatua ya lazima kwa sababu ya ongezeko la kesi za ubakaji wa watoto. Kwa mujibu wa waziri huyo, mnamo 2023, kesi 600 za ubakaji wa watoto zilirekodiwa, na kwamba 133 tayari zimeripotiwa katika mwezi Januari pekee mwaka huu.
 
"Madagascar ni nchi huru ambayo ina haki ya kurekebisha sheria zake kuhusiana na mazingira na maslahi ya jumla ya watu," amesema Randriamanantenasoa na kuongeza kuwa sheria ya sasa ya adhabu haijatosha kuwadhibiti wahalifu wa makosa hayo.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, kuhasiwa kwa upasuaji kutatekelezwa kwa wanaopatikana na hatia ya kubaka mtoto wa chini ya umri wa miaka 10. Kesi za ubakaji watoto kati ya umri wa miaka 10 na 13 zitaadhibiwa kwa upasuaji au kuhasiwa kwa kemikali. Ubakaji wa watoto kati ya miaka 14 na 17 utaadhibiwa kwa kuhasiwa kwa kemikali.

 
Wahalifu wanaweza wakakabiliwa na adhabu kali za hadi kifungo cha maisha jela pamoja na kuhasiwa.
 
Kuhasiwa kwa kemikali kunafanyika kwa kutumia vidonge.
 
Nchi kadhaa na baadhi ya majimbo ya Marekani - ikiwa ni pamoja na California na Florida - huruhusu wahalifu kuhasiwa kwa kemikali kwa baadhi ya makosa ya ngono. 
 
Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto na mashirika mengine mara kwa mara yamekuwa yakiangazia viwango vya juu vya udhalilishaji wa kingono dhidi ya watoto nchini Madagascar.
 
Baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yanasema idadi halisi ya ubakaji wa watoto ni kubwa zaidi kuliko takwimu rasmi, lakini kesi nyingi haziripotiwi kwa sababu ni suala la mwiko na waathiriwa mara nyingi huona aibu.../
 
 
 
 

Tags