Dec 09, 2023 11:14 UTC
  • Soka Afrika: Uganda kidedea Cecafa U18

Timu ya taifa ya soka ya vijana ya Uganda imebuka kidedea baada ya kuichabanga Kenya mabao 2-1 katika fainali ya Mashindano ya Kandanda ya Kanda ya Afrika Mashariki na Kati Cecafa kwa vijana wenye chini ya miaka 18.

Katika fainali hiyo iliyopigwa katika Uwanja wa Jomo Kenyatta mjini Kisumu, magharibi mwa Kenya siku ya Ijumaa, timu hizo mbili zilikabana koo katika kipindi cha kwanza na kushindwa kutikisa nyavu za hasimu.

Wenyeji walitangulia kuona lango la wageni katika kipindi cha pili, kupitia goli la Syphas Owuor kunako dakika ya 65 ya mchezo, lakini Uganda wakasawazisha dakika 10 baadaye, kupitia Batiibwe Okello.

Hakim Mutebi alivurumisha kombora lililotikisa nyavu za wenyeji, kwenye dakika za nyongeza baada ya dakika 90 za ada kuishia kwa sare ya bao 1-1, na kuifanya Uganda itwae ubingwa wa Kombe la Cecafa kwa vijana wenye chini ya miaka 18 kwa mwaka huu 2023.

Junior Stars walifuzu kwa fainali hizo Jumanne, Desemba 5, 2023 baada ya kuibwaga Tanzania 4-3 kupitia kwa mikwaju ya penalti baada ya timu hizo kutofungana katika muda wa kawaida wa dakika 90, pamoja na muda wa ziada wa dakika 30.

Uganda nao walifuzu baada ya kushinda Rwanda kwa bao lililofungwa na Abubakar Mayanja, ambalo limezua utata miongoni mwa mashabiki kwa madai kwamba Mayanja alipachika bao hilo wavuni akiwa ameotea.

Tags