Mawakili Kenya katika mgomo wa siku 5 kulalamikia kuuawa mwenzao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10600-mawakili_kenya_katika_mgomo_wa_siku_5_kulalamikia_kuuawa_mwenzao
Maelfu ya mawakili nchini Kenya jana Jumatatu walitangaza mgomo wa siku tano wa kususia vikao mahakamana kufuatia kuuawa wakili mwenzao ambaye mwili wake ulipatikana ukiwa umetupwa kwenye mto kusini mashariki mwa mji mkuu, Nairobi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 05, 2016 03:51 UTC
  • Mawakili Kenya katika mgomo wa siku 5 kulalamikia kuuawa mwenzao

Maelfu ya mawakili nchini Kenya jana Jumatatu walitangaza mgomo wa siku tano wa kususia vikao mahakamana kufuatia kuuawa wakili mwenzao ambaye mwili wake ulipatikana ukiwa umetupwa kwenye mto kusini mashariki mwa mji mkuu, Nairobi.

Miili ya wakili, mteja wake na dereva wake wa taxi ilipatikana ikiwa imekatakatwa na kutupwa mtoni jambo ambalo limeibua hasira miongoni mwa mawakili na watetezi wa haki za binadamu.

Mbali na mgomo huo, mawakili wameitisha maandamano ya amani katika miji mbali mbali kote nchini Kenya huku wakitaka serikali iharakishe mashtaka dhidi ya waliohusika na mauaji ya watatu hao.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mawakili wa Kenya, Isaac Okero, amesema mgomo huo wa wiki moja unalenga kushinikiza kupatikana ukweli kuhusu kutoweka na kisha kuuawa wakili aliyekuwa na umri wa miaka 31, Willy Kimani. Amesema limekuwa ni jambo la kawaida kwa Wakenya kutoweka na kuuawa kiholela jambo ambalo haliwezi kukubalika tena.

Mkuu wa Polisi ya Kenya Jumamosi aliwataja maafisa watatu wa polisi ambao ni washukiwa wakuu katika mauaji hayo. Wakili huyo alikuwa akimuwakilisha mteja wake ambaye alikuwa ameishtaki polisi kwa kumpiga risasi na kumjeruhi.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights yamelaani mauaji ya watatu hao na kutaka uchunguzi kamili ufanyike.