Dec 18, 2023 07:05 UTC
  • Mvutano waongezeka huku uchaguzi ukikaribia Congo DR

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inajiandaa kwa ajili ya uchaguzi Jumatano ambao ima utaimarisha demokrasia yake au kuzua ghasia mpya huku mivutano ya kisiasa ikiongezeka na kutishia amani na usalama wa nchi hiyo.

Takriban wapiga kura milioni 44 waliojiandikisha wanatazamiwa kupiga kura mnamo Desemba 20 katika taifa hilo kubwa la Afrika ya kati lenye takriban watu milioni 100 katika uchaguzi wa rais, bunge, majimbo na mabaraza ya mitaa.

Takriban watu 100,000 wanagombea katika kura hizo nne, huku Rais Felix Tshisekedi akitafuta muhula mwingine baada ya kushinda uchaguzi uliokuwa na utata mwaka 2018.

Ukubwa wa DRC, ambao ni takriban sawa na bara la Ulaya Magharibi, unafanya kuandaliwa uchaguzi kuwa jambo gumu na zito.

Nchi hiyo pia licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili, ni mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani na ina miundombinu duni, huku tume ya uchaguzi ya CENI ikikabiliwa na matatizo makubwa katika kusambaza vifaa vya kupigia kura katika zaidi ya vituo 175,000.

Gaucher Kizito Mbusa mtaalamu wa masuala ya kisiasa amesema upigaji kura unatarajiwa kufanyika bila matatizo katika maeneo yenye watu wengi zaidi lakini itakuwa vigumu katika maeneo ya vijijini kutokana na ukosefu wa usalama na barabara mbovu.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa  Ijumaa lilipasisha ombi la serikali kwamba ujumbe unaomaliza muda wake wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO, utoe msaada wa vifaa zaidi ambako wametumwa katika majimbo matatu ya mashariki yaliyokumbwa na ghasia.

Mwanadiplomasia mmoja amesema kwamba sio vituo vyote vya kupigia kura vitafunguliwa mnamo Desemba 20 kutokana na ukosefu wa vifaa,  na kuwa vinaweza kufunguliwa siku moja au mbili baada ya kuanza uchaguzi.

Katika ripoti yake Jumamosi, Human Rights Watch (HRW) ilionya kuhusu ghasia za uchaguzi ambazo zinaweza kuhatarisha upigaji kura.

Wagombea muhimu wa urais ni pamoja na Moise Katumbi, tajiri mkubwa na gavana wa zamani wa mkoa ambaye anaungwa mkono na wagombea wanne wa zamani.

Wawaniaji wengine wa upinzani ni Martin Fayulu, mtendaji mkuu wa zamani wa sekta ya mafuta ambaye anadai alishinda uchaguzi wa 2018, na Denis Mukwege, daktari ambaye alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel kwa kushughulikia waathiriwa wa ubakaji.

Huku kukiwa na idadi mdogo ya wapigaji kura, baadhi ya waangalizi wanaamini kuwa Tshisekedi na Katumbi ndio wanaoweza kuwa mstari wa mbele kwa kuzingatia rasilimali zao na wafuasi wengi wakati wa kampeni.

Tshisekedi anaonekana kuwa na nafasi nzuri ya kushinda kwa kuzingatia kutokea mgawanyiko katika mrengo wa upinzani.

Kampeni za uchaguzi zinamalizika rasmi leo Jumatatu.