Jan 13, 2024 06:16 UTC
  • Baada ya Mauritius na Algeria, Cape Verde yawa nchi ya tatu barani Afrika kutokomeza Malaria

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeitangaza Cabo Verde kuwa nchi isiyo na Malaria kwa kufanikiwa kuutokomeza ugonjwa huo na kuipatia cheti rasmi cha uthibitisho.

Sherehe za utoaji cheti hicho zimefanyika jijini Geneva Uswisi katika makao Makuu ya WHO ambapo nchi hiyo imekuwa moja kati ya nchi 43 na mamlaka moja zilizofanikiwa kutokomeza ugonjwa huo hatari unaosababisha vifo vya mamilioni ya watu kila mwaka hususan barani Afrika. 

Akikabidhi cheti hicho Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ameipongeza Cabo Verde kwa kufanikiwa katika vita vya kimataifa dhidi ya malaria, na kusema nchi hiyo imetoa matumaini kwamba kwa kutumia zana zilizopo pamoja na mpya, zikiwemo chanjo, dunia inaweza kuthubutu kuwa na ndoto ya ulimwengu usio na malaria.

Dkt. Tedros Adhanom amesema: “Ninaipongeza serikali na watu wa Cabo Verde kwa kujitolea kwao bila kuyumbayumba na kwa ustahimilivu katika safari yao ya kutokomeza malariaa. Cheti cha uthibitisho cha WHO kwa Cabo Verde kuwa haina malaria ni uthibitisho wa nguvu ya upangaji mkakati wa afya ya umma, ushirikiano, na juhudi endelevu za kulinda na kukuza afya".

Kisiwa cha Cabo Verde, chenye muunganiko wa visiwa 10 katika Bahari ya Atlantiki ya Kati, kilikuwa kikikabiliwa na changamoto kubwa za malaria. Kabla ya miaka ya 1950, visiwa vyote viliathiriwa na malaria. Miripuko mikali ya malaria ilikuwa ikitokea mara kwa mara katika maeneo yenye watu wengi hadi hatua zilizolengwa kumaliza tatizo hilo zilipotekelezwa. 

Ulisses Correia e Silva

Akiishukuru WHO kwa kuitambua rasmi Cabo Verde kuwa nchi isiyo na malaria, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Ulisses Correia e Silva amesema “kuthibitishwa kwetu kuwa nchi isiyo na malaria kuna athari kubwa chanya, na imechukua muda mrefu kufikia hatua hii. Kwa upande wa sura ya nje ya nchi, hili ni jambo zuri sana kwa utalii na kwa kila mtu mwingine. Changamoto ambayo Cabo Verde imeshinda  katika mfumo wa afya inatambulika”.

Mzigo wa malaria ndio mkubwa zaidi katika bara la Afrika, ambapo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, bara hilo lilichangia karibu asilimia 95 ya wagonjwa wa malaria duniani na asilimia 96 ya vifo vinavyohusiana na ugonjwa huo kwa mwaka 2021.

Cabo Verde yenye idadi ya watu wapatao laki tano, ni nchi ya tatu kuthibitishwa kuwa imetokomeza ugonjwa wa malaria katika kanda ya Afrika, ikiungana na Mauritius iliyothibitishwa mwaka 1973 na Algeria ambayo ilikabidhiwa cheti cha uthibitisho mwaka 2019.../

Tags