Jan 17, 2024 02:35 UTC
  • Sudan 'yasimamisha' ushirikiano na jumuiya ya IGAD

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imetangaza kusimamisha ushirikiano na Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD), hatua ambayo wadadisi wa mambo wanasema inaashiria kugonga mwamba jitihada za hivi punde za kieneo za kuhitimisha vita katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Taarifa ya jana Jumanne ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan imesema taifa hilo halitafanya majadiliano yoyote na IGAD kuhusu suala lolote linalohusu Sudan.

Tangazo hilo limekuja saa chache kabla ya kuanza mkutano wa jumuiya hiyo ya kieneo ya Afrika Mashariki huko mjini Entebbe nchini Uganda, kujadili mgogoro wa Sudan. 

Aidha haya yanajiri siku chache baada ya Jeshi la Sudan kukataa kushiriki mkutano wa ngazi ya juu wa IGAD wa kuzindua mchakato wa amani wa nchi hiyo, uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia; huku mapigano yakishtadi katika nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.

Sudan imekuwa ikishuhudia mapigano makali kati ya majenerali wa kijeshi wenye uchu wa madaraka ambao wanaongoza makundi mawili ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Radiamali ya Haraka, RSF tangu Aprili 15, 2023.

Mapigano Sudan

Mapigano hayo hadi sasa yameshasababisha zaidi ya watu 1,200, kuuawa kama zinavyoonesha takwimu za Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu OCHA. Baadhi ya duru zinasema waliouawa ni zaidi ya 1,300.

Aidha kwa mujibu wa taasisi hiyo ya UN, idadi ya watu waliokimbia vita nchini Sudan imeshapindukia milioni 7.4, tangu mapigano yalipozuka kati ya SAF na wapiganaji wa RSF mnamo Aprili 15, 2023.

Tags