Jan 30, 2024 11:30 UTC
  • ICC: Tunaamini pande zote mbili za vita nchini Sudan zimefanya uhalifu wa kivita Darfur

Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, Karim Khan, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba kuna "sababu za kuamini" kwamba jeshi la Sudan, Vikosi vya Msaada wa Haraka, na vikundi washirika wao wamefanya uhalifu wa kivita huko Darfur.

Karim Khan ameyasema hayo wakati akiwasilisha ripoti kuhusu ukiukaji wa sheria unaofanyika huko Darfur, magharibi mwa Sudan.

Khan ameliambia Baraza la Usalama kwamba ukatili uliotokea El Geneina, Darfur Magharibi, ni msingi muhimu wa uchunguzi unaofanywa na taasisi hiyo, akisisitiza kwamba timu yake bado inakusanya ushahidi na taarifa kuhusu uhalifu uliofanyika huko Darfur.

Karim Khan alialianzisha uchunguzi wa uhalifu wa kivita Julai mwaka jana baada ya kuongezeka vitendo vya uhasama katika eneo la Darfur.

Karim Khan

Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa uliochapishwa Januari 20 ulisema kuwa kati ya watu 10,000 na 15,000 waliuawa mwaka jana katika mji wa El Geneina, kutokana na mapigano ya kikabila na ukatili uliofanywa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na wanamgambo wanaoshirikiana na kundi hilo. 

Akizungumza mbele ya Baraza la Usalama, Khan ameripoti kwamba wakimbizi kutoka Darfur katika kambi za wakimbizi alizotembelea Jumamosi iliyopita nchini Chad walimtolea ushuhuda unaoelezea unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana huko Darfur, mauaji ya kikatili, na uhalifu unaosababishwa na ubaguzi wa rangi. 

Chad inawapa hifadhi zaidi ya wakimbizi 540,000 wa Sudan, na ripoti za Umoja wa Mataifa zinasema idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi 910,000 kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Tags