Upinzani Afrika Kusini wataka kura zihesabiwe upya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i112418-upinzani_afrika_kusini_wataka_kura_zihesabiwe_upya
Taharuki imetanda Afrika Kusini baada ya vyama kadhaa vya upinzani nchini humo kupinga matokeo ya uchaguzi wa Bunge katika baadhi ya wilaya na mikoa, vikisisitiza kuwa lazima kura zihesabiwe upya.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
May 31, 2024 23:36 UTC
  • Upinzani Afrika Kusini wataka kura zihesabiwe upya

Taharuki imetanda Afrika Kusini baada ya vyama kadhaa vya upinzani nchini humo kupinga matokeo ya uchaguzi wa Bunge katika baadhi ya wilaya na mikoa, vikisisitiza kuwa lazima kura zihesabiwe upya.

Vyama hivyo vikiongozwa na Democratic Alliance (DA) vimesema ujumlishaji wa matokeo katika baadhi ya maeneo hasa katika mkoa wa Western Cape umekumbwa na mizingwe na uchakachuaji, na hivyo vinataka kura zihesabiwa tena.

Mvutano kuhusu matokeo katika mkoa huo uliilazimisha Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini (IEC) kuakhirisha kutangaza matokeo ya uchaguzi katika mkoa huo jana usiku, na inatazamiwa kutangaza leo asubuhi.

Kwa mujibu wa asilimia 96 ya matokeo yaliyochapishwa kwenye tovuti ya Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini (IEC), chama tawala ANC kinaongoza kwa kuzoa asilimia 39.86 ya kura, kikifuatiwa na chama cha Democratic Alliance (DA) kilichozoa asilimia 21.65, huku chama kipya cha Mkhonto weSizwe (MK) cha rais wa zamani, Jacob Zuma kikiambulia asilimia 14.5 ya kura.

Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Julius Malema ambacho kilitazamiwa kutoa ushindani mkubwa dhidi ya chama tawala, kimezoa asilimia 9.54 ya kura. 

Licha ya kuwa kifua mbele, lakini chama cha ANC,  kinaelekea kupoteza wingi wa viti bungeni kwa mara ya kwanza tangu 1994, ambapo umashuhuri wake umeshuka hadi chini ya asilimia 40 ikiwa ni upungufu mkubwa wa asilimia 15 wa uungwaji mkono. Kwa matokeo haya, ANC italazimika kuingia katika muungano wa kitaifa na ama chama cha Democratic Alliance (DA), Economic Freedom Fighters (EFF) au Mkhonto weSizwe (MK).

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Sizwe Mpofu-Walsh amenukuliwa na kanali ya televisheni ya al-Jazeera akisema, "Matokeo haya yanaashiria mwisho wa umaarufu na ushawishi wa ANC."