Watu 120 wameuawa mjini el-Fasher, Sudan ndani ya wiki 2
Kwa akali watu 123 wameuawa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita katika mapigano yanayoendelea kushuhudiwa katika mji wa el-Fasher, jimboni Darfur, magharibi mwa Sudan.
Hayo yalisemwa jana Jumapili na Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) na kuongeza kuwa, mapigano hayo kati ya jeshi la serikali na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) pia yamepelelekea watu 930 kujeruhiwa katika mji huo, ambayo ni makao makuu ya mkoa wa Darfur Kaskazini.
Taarifa ya MSF imeeleza kuwa: Hii ni alama ya kushtadi mapigano mjini el-Fasher. Tunaziomba pande hasimu kufanya kila wawezalo kuwalinda raia."
Wakati huo huo, Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, amesema kwamba "ameshtushwa" na ongezeko la ghasia katika mji huo wa magharibi mwa Sudan.
Amewaonya makamanda wa pande mbili kwamba mapigano katika mji wa el-Fasher yatasababisha maafa na kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu nchini Sudan hasa jimboni Darfur.
Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka jana kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF) linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na wanamgambo wa RSF ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo.
Hadi sasa juhudi za upatanishi wa kimataifa za kuhitimisha mapigano hayo ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 14,000 na takriban milioni 8.5 kulazimika kuwa wakimbizi ndani ya nje ya Sudan, zimegonga mwamba.