Jeshi la Sudan lapuuzilia mbali mwito wa Marekani
Jeshi la Sudan limepinga mwito wa Marekani wa kurejea kwenye meza ya mazungumzo kati ya jeshi hilo na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).
Malik Agar, kiongozi wa zamani wa waasi ambaye hivi sasa ni kiongozi nambari mbili katika Baraza la Mpito la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan amesema: Hatutaenda Jeddah (Saudi Arabia kwa ajili ya mazungumzo), na yeyote anayetaka twende, atuue kwenye nchi yetu kisha apelekea maiti zetu huko (Jeddah).
Matamshi ya Agar yamekuja kufuatia mazungumzo yaliyofanyika baina al-Burhan na Antony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, ambapo Washington imetaka kuendelea mazungumzo ya Jeddah yaliyokwama kwa miezi kadhaa sasa baada ya kukosa kufikia tija yoyote.
Haya yanajiri huku mapigano makali yakiendelea katika mji wa el-Fasher, jimboni Darfur, magharibi mwa Sudan. Jumapili iliyopita, Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) ilisema kwa akali watu 123 wameuawa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita katika mapigano yanayoendelea kushuhudiwa katika mji wa el-Fasher.
Kwa mujibu wa MSF, mapigano hayo kati ya jeshi la serikali na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) pia yamepelelekea watu 930 kujeruhiwa katika mji huo, ambayo ni makao makuu ya mkoa wa Darfur Kaskazini.
Hadi sasa juhudi za upatanishi wa kimataifa za kuhitimisha mapigano hayo yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka jana na ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 14,000 na takriban milioni 9 kulazimika kuwa wakimbizi ndani ya nje ya Sudan, zimegonga mwamba.