Feb 12, 2024 04:38 UTC
  • 'Washauri wa kijeshi' wa Imarati, Bahrain wauawa na al-Shabaab Somalia

Kwa akali wakufunzi watano wa kijeshi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Bahrain wameuawa katika shambulizi linaloaminika kufanywa na wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab huko Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.

Rais Hassan Sheikh Mohamoud wa Somalia huku akithibitisha ripoti za kuuawa 'washauri hao wa kijeshi' wa Imarati na Bahrain, ametoa mwito wa kuchukuliwa hatua kali wahusika wa hujuma hiyo.

Wizara ya Ulinzi ya Imarati imesema katika taarifa kuwa, miili ya wakufunzi wanne wa kijeshi waliouawa katika shambulio hilo dhidi ya chuo cha mafunzo ya kijeshi cha Jenerali Gordon mjini Mogadishu iliwasili jana Jumapili mjini Abu Dhabi. Mkufunzi wa tano aliyeuawa katika hujuma hiyo ya Jumamosi ni raia wa Bahrain.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Garowe, aliyehusika na shambulio hilo tayari alikuwa ndani chuo hicho cha kijeshi jijini Mogadishu, na haijabainika aliwezaje kuingia kwenye kambi hiyo yenye ulinzi mkali.

Wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab

Rais Hassan Sheikh Mohamoud wa Somalia ameviagiza vyombo vya usalama vya nchi hiyo vifanye uchunguzi wa kina mara moja, ili kuwabaini wapangaji wa shambulio hilo la kigaidi.

Habari zaidi zinasema kuwa, aliyetekeleza shambulio hilo, aliingia kinyemela kambini hapo na kuanza kufyatua risasi ovyo, huku akiwalenga zaidi washauri wa kijeshi wa Imarati na Bahrain.

Tayari genge la kigaidi la al-Shabaab ambalo tokea mwaka 2007 limekuwa likifanya mashambulizi dhidi ya maafisa usalama na raia nchini Somalia na vile vile dhidi ya askari wa kigeni nchini humo, limetangaza kuhusika na hujuma hiyo ya Jumamosi.

 

Tags