Feb 20, 2024 12:52 UTC
  • Watawala wa kijeshi Guinea watangaza kuvunja serikali ya mpito

Utawala wa kijeshi wa Guinea Conakry ambao ulitwaa madaraka kupitia mapinduzi zaidi ya miaka miwili iliyopita, umetangaza kuvunja serikali ya mpito ya nch hiyo ya Afrika Magharibi.

Katika ujumbe wa video, vingozi hao wa kijeshi nchini Guinea hawajatoa sababu za kuivunja serikali hiyo ya muda, lakini wamesema watateua serikali mpya karibuni hivi.

Taarifa hiyo ya jana Jumatatu imeeleza kuwa, wakurugenzi wa baraza la mawaziri, makatibu wakuu na manaibu wao ndio watakaoiongoza serikali hiyo ya mpito hadi pale serikali mpya itakapoteuliwa.

Serikali hiyo ya muda imekuwepo madarakani tokea Julai mwaka 2022. Ikumbukwe kuwa, kiongozi wa kijeshi wa Guinea, Kanali Mamady Doumbouya, alichukua mamlaka katika mapinduzi ya kijeshi ya mwaka wa 2021, na kumuondoa madarakani Rais Alpha Condé.

Kanali Mamady Doumbouya

Guinea ni miongoni mwa nchi kadhaa za magharibi na katikati mwa Afrika ambazo zimeshuhudia mapinduzi katika miaka ya hivi karibuni pamoja na Mali, Burkina Faso, Niger na Gabon. 

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) zililaani mapinduzi hayo, licha ya kuonekana kuungwa mkono na wananchi wa mataifa hayo.

Tags