Mar 04, 2024 10:45 UTC
  • Khartoum yakanusha madai kuwa Iran inataka kujenga kambi ya kijeshi Sudan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan amekadhibisha madai ya gazeti moja la Marekani kwamba Iran imeiomba serikali ya Sudan idhini ya kujenga kituo cha kudumu cha kijeshi katika maji ya Bahari Nyekundu, pwani ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Ali Al-Sadiq Ali amenukuliwa na shirika la habari la Sputnik kitengo cha lugha ya Kiarabu akikanusha madai hayo aliyosisitiza kuwa haya msingi, pambizoni mwa mkutano wa Jukwaa la Diplomasia la Antalya, kusini magharibi mwa Uturuki.

Ali amesema, "Nimesoma makala iliyochapishwa na gazeti la Marekani la Wall Street Journal. Habari iliyochapishwa ni ya urongo na uzushi. Iran haijawahi kuiomba Sudan (idhini ya) kujenga kambi ya kijeshi."

Waziri huyo wa Sudan amesema hivi karibuni aliitembelea Iran na suala hilo la eti Iran kutaka kujenga kituo cha kudumu cha kijeshi katika pwani ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika halikujadiliwa.

Gazeti la Marekani la Wall Street Journal lilidai katika ripoti yake hiyo kuwa, Iran imeahidi kuipa Sudan silaha na zana za kisasa za kijeshi ikiwemo manowari yenye uwezo wa kubebe helikopta, mkabala wa kuruhusiwa kujenga kambi ya kijeshi katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Uhusiano wa Iran na nchi za Afrika unazitia kiwewe nchi za kibeberu na Kizayuni

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan aliitembelea Iran mwezi Februari mwaka huu, na kukutana na kuzungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Jamhuri ya Kiislamu katika ziara rasmi ya hapa Tehran. Hiyo ilikuwa ni ziara ya kwanza ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan kuitembelea Tehran baada ya kusitishwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili mwaka 2015.

Kufuatia shambulio dhidi ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Tehran na ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Mashhad yaliyotokea mwezi Januari 2014, Sudan iliungana na Saudia kukata uhusiano wao wa kidiplomasia na Iran lakini hivi sasa nchi hizo zote zimerejesha uhusiano wao na Jamhuri ya Kiislamu.

 

Tags