Makubaliano ya viongozi wa Libya ya kuunda serikali moja mpya
Kuendelea mgogoro nchini Libya na kuwa vigumu suala la kufanyika uchaguzi nchini humo hatimaye kumepelekea viongozi wa Libya kukubaliana kuunda serikali moja ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia uchaguzi nchini humo.
Katika mkutano uliofanyika huko Benghazi, Mohammad Menfi Mwenyekiti wa Baraza la Rais, Mohammad Tekala Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Serikali na Aguila Saleh Issa, Spika wa Bunge, wametangaza kwamba kuna haja ya kuundwa serikali moja mpya ambayo itasimamia uchaguzi ulioahirishwa.
Katika taarifa yao ya pamoja viongozi hao watatu wa Libya pia wameutaka ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulioko nchini humo na jamii ya kimataifa kuunga mkono mapendekezo yao. Vilevile wamefikia makubaliano ya kuunda kamati ya kiufundi kwa ajili ya kuchunguza masuala yenye utata katika uwanja huo.
Nchi ya Libya bado inakabiliwa na matatizo ya kisiasa, tofauti za kimitazamo, uchu wa madaraka na uingiliaji wa kigeni, ikiwa imepita zaidi ya miaka 13 tangu kuanza mzozo wa kisiasa nchini humo.
Hali ya kisiasa na tofauti za mitazamo zimepelekea nchi hiyo kukosa serikali kuu yenye nguvu kwa ajili ya kuandaa uchaguzi wa kumchagua rais wa nchi hiyo. Ijapokuwa mashirika ya kimataifa yamefanya jitihada nyingi kwa ajili ya kumaliza mgogoro wa Libya na makundi ya kisiasa kutangaza kuwa tayari kuandaa uchaguzi, lakini kivitendo tofauti za maoni zimekuwa zikizidisha mzozo wa kisiasa na hivyo kutia dosari uwezekano wa kufanyika uchaguzi huo.
Kuhusiana na hilo, ilikuwa imepangwa uchaguzi wa bunge na rais ufanyika mwishoni mwa 2021, lakini ukaahirishwa kutokana na vikwazo vya kisheria na kutokuwepo miundombinu muhimu nchini.
Abdoulaye Bathily, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amesema kuhusu suala hilo: Kuwepo serikali moja nchini Libya ni jambo muhimu sana kwa ajili ya kurudishwa amani na utulivu. Kwa hakika makundi ya kisiasa ya Libya yanajaribu kufikia suluhu ili kukomesha mgogoro wa kisiasa nchini baada ya kupita zaidi ya miaka 13 tokea kupinduliwa Muammar Gaddafi, dikteta wa zamani wa nchi hiyo.
Jambo hilo kwa kuzingatia hali ya kisiasa inayotawala nchini limekuwa changamoto kubwa kwa viongozi wa makundi ya kisiasa kwa kutilia maanani kuongezeka hatari ya nchi za kigeni kuingilia masuala ya ndani ya Libya, pamoja na uwezekano wa kuimarishwa harakati za makundi ya kigaidi katika nchi hiyo. Vita vya Gaza, Ukraine na kuvurugika hali ya kisiasa katika eneo, soko la nishati, hali ya nchi za Ulaya na kuongezeka idadi ya wakimbizi wanaoelekea Ulaya kupitia nchi hiyo ni mamabo ambayo yamewapelekea viongozi wa Libya na makundi mbalimbali kuwa na wasiwasi zaidi kuhusiana na mustakabali wa nchi hiyo kuliko hapo awali.
Aguila Saleh Issa, Spika wa Bunge la Libya, amesema kuhusu suala hilo kwamba mgogoro wa nchi hiyo utatatuliwa kupitia uchaguzi wa bunge na rais, kwa sababu ni katika kivuli hicho tu ndipo nguvu ya utendaji itawekwa sehemu moja. Ingawa makundi ya kisiasa ya Libya yametangaza azma yao ya kufanya uchaguzi na kuitikia mwito wa kuundwa serikali moja, lakini bado kuna vizingiti vingi kabla ya kufikiwa jambo hilo.
Ingawa vyama vya kisiasa vya Libya vinajaribu kudhibiti hali ya mambo, lakini tofauti za kisiasa bado zinajitokeza nchini. Kadhalika, uingiliaji kati wa moja kwa moja na usiokuwa wa moja kwa moja na himaya ya nchi za kigeni kwa baadhi ya makundi ya kisiasa nchini Libya na matakwa yao ya kushirikishwa katika muundo wa kisiasa yamefanya masuala ya nchi hiyo kuwa magumu.
Inaonekana kuwa bado kuna vikwazo vingi vinavyozuia kufanyika uchaguzi na kukomeshwa machafuko na vita katika nchi hiyo, jambo ambalo linafanya kutabirika hali ya nchi hiyo kuwa kugumu. Bathily, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amesema: 'Hali ya hivi sasa inatufanya tutoe kipaumbele kwa haja ya kufikiwa makubaliano ambayo yataandaa uwanja wa kufanyika uchaguzi na kuunganishwa taasisi za serikali nchini Libya.'