Mar 20, 2024 02:43 UTC
  • Niger ilivunja mkataba wa kijeshi na Marekani baada ya 'kuonywa' kuhusu uhusiano wake na Iran, Russia

Serikali ya Niger iliamua kusitisha makubaliano ya kijeshi na Marekani baada ya ujumbe wa maafisa wakuu wa kijeshi wa Marekani kuitembelea nchi hiyo ya Afrika Magharibi na "kueleza wasiwasi" kuhusu uhusiano wake na Russia na Iran unaokua

Pentagon ilisema Jumatatu kwamba maafisa hao walisafiri hadi mji mkuu wa Niamey wiki iliyopita ili kujadili suala hilo na uongozi wa kijeshi wa nchi hiyo, wakitaka ufafanuzi kuhusu mipango ya baadaye.

Msemaji wa Pentagon Sabrina Singh alidai kuwa serikali ya Marekani ilikuwa na mazungumzo ya "moja kwa moja na ya wazi" nchini Niger, na inaendelea kuwasiliana na baraza tawala la kijeshi la nchi hiyo - linalojulikana kama Baraza la Kitaifa la Ulinzi wa Nchi (CNSP).

Singh amesema: "Maafisa wa Marekani walionyesha wasiwasi wao juu ya uwezekano wa uhusiano wa Niger na Russia na Iran."

Serikali ya Niger ilitangaza siku ya Jumamosi kwamba  imefuta makubaliano ya ushirikiano wa ulinzi wa 2012 na Marekani.

Uamuzi huo umechukuliwa siku chache baada ya ujumbe wa ngazi ya juu wa Marekani, uliojumuisha Mkuu wa Kamandi ya nchi hiyo barani Afrika, Jenerali Michael Langley, kukamilisha ziara yake ya siku tatu katika taifa hilo la Afrika.

Ndege ya kivita ya Marekani ikiwa katika kituo cha kijeshi cha Agadez nchini Niger

Kwa mujibu wa Kanali Abdramane, Niger imesikitishwa na nia iliyoonyeshwa na ujumbe wa Marekani ya kuwanyima watu huru wa Niger haki ya kuchagua washirika wao na aina ya ushirikiano wenye uwezo wa kuwasaidia kikwelikweli kupambana na ugaidi, na akaongeza kuwa Wamarekani hawakufuata itifaki ya kidiplomasia walipoelekea Niger na hata hawakuwafahamisha wenyeji wao kuhusu ajenda ya mazungumzo na tarehe ya kuwasili kwao.

Marekani ingali imeweka wanajeshi wake1,000 nchini Niger kwenye kituo cha ndege zisizo na rubani kilichojengwa kwa gharama ya dola milioni 100.

Maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi wa Russia akiwemo Naibu Waziri wa Ulinzi Yunus-bek Yevkurov, wametembelea Niger na kukutana na uongozi wa kijeshi wa nchi hiyo.

Waziri mkuu wa Niger Ali Mahamane Lamine Zeine, naye alitembelea Iran mwezi Januari.

Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Niger, Bakary Yaou Sangare, alitembelea Tehran mnamo Oktoba 2023 ili kutafuta fursa za kuimarisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi, na pia kuongeza ushirikiano katika sekta za sayansi na teknolojia kati ya nchi hizo mbili.

Tags