May 10, 2024 07:23 UTC
  • Iran: Lugha ya Kifarsi kufundishwa katika Vyuo Vikuu vya Zimbabwe

Waziri wa Sayansi, Utafiti na Teknolojia wa Iran ametangaza utayarifu wa Jamhuri ya Kiislamu wa kuanza kufunza lugha ya Kifarsi katika Vyuo Vikuu vya Zimbabwe.

Mohammad Ali Zulfi Gol, Waziri wa Sayansi, Utafiti na Teknolojia wa Iran amesema hayo katika mkutano wake na Profesa Amon Murwira, Waziri wa Elimu ya Juu, na Ustawi wa Sayansi na Teknolojia wa Zimbabwe katika Wizara ya Sayansi, Utafiti na Teknolojia ya Iran.

Zulfi Gol ameashiria safari ya Rais Ebrahim Raisi wa Iran nchini Zimbabwe mwaka jana na kueleza kuwa, uhusiano baina ya nchi mbili hizi ni wa kirafiki na wenye umuhimu mkubwa sana.

Ameongeza kuwa, Zimbabwe ina madini na maliasili zenye thamani, na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaweza kuipa nchi hiyo ya Kiafrika ujuzi wake wa sayansi na teknolojia ili iweze kustafidi kikamilifu na madini hayo.

Gol amegusia nafasi ya lugha na fasihi katika kuyakurubisha pamoja mataifa na kueleza bayana kuwa: Iran ipo tayari kuzindua kozi za lugha ya Kifarsi na fasihi katika Vyuo Vikuu vya Zimbabwe, sambamba na kugharamia karo na kuwatuma maprofesa wake (nchini Zimbabwe), na pendekezo hili limekubaliwa na kupokolewa vizuri na Waziri wa Elimu ya Juu, na Ustawi wa Sayansi na Teknolojia wa Zimbabwe.  

Lugha ya Kifarsi (Kifursi au Kiajemi), ambayo ni lugha rasmi na ya taifa nchini Iran, hivi sasa inafunzwa katika zaidi ya Vyuo Vikuu 200 duniani.

Kustawisha uhusiano na nchi za Kiafrika katika nyuga mbali bali imekuwa stratijia ya Iran tangu ulipopatikana Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979.

Tags