Maiti 65 za wahajiri zagunduliwa katika kaburi la umati Libya
(last modified Sat, 23 Mar 2024 07:50:38 GMT )
Mar 23, 2024 07:50 UTC
  • Maiti 65 za wahajiri zagunduliwa katika kaburi la umati Libya

Maafisa wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) wameripoti kuwa wamegundua miili ya watu 65 iliyokuwa imezikwa kwenye kaburi la umati nchini Libya.

IOM bila kueleza kuhusu uraia na mazingira ya kufariki dunia wahajiri hao huko kusini magharibi mwa Libya, imesema serikali ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika inachunguza kiini cha vifo hivyo.

Sambamba na kusema kuwa limesikitishwa na kushtushwa na ugunduzi huo, shirika hilo la kimataifa limesema: Gharama ya kutochukua hatua imedhihirika katika kuogezeka vifo vya binadamu, na hali ya kutamausha wanayopitia wakimbizi.

Haya yanajiri chini ya wiki mbili baada ya wahajiri 60 kufa maji baada ya boti yao kuzama kwenye Bahari ya Mediterania, katika mji wa pwani wa Zawiya, kaskazini magharibi mwa Libya.

Kwa mujibu wa IOM, wahamiaji haramu 17,025 waliokolewa na kurudishwa Libya kuanzia mwezi Januari hadi Disemba, mwaka uliopita wa 2023. Aidha takwimu za shirika hilo la Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa wahamiaji 974 walikufa maji na 1,372 walipotea kwenye Bahari ya Mediterania katika pwani ya Libya mwaka 2023.

Wahajiri wanavyohatarisha maisha yao kwenda Ulaya kupitia usafari wa baharini

Libya imekuwa njia kuu inayotumiwa na wahamiaji haramu kutokana na kukosekana na serikali kuu tangu ulipoangushwa utawala wa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011. Wengi wa wahamiaji hao haramu ni raia wa nchi za Afrika za kusini mwa Jangwa la Sahara na wanahatarisha maisha yao kwa tamaa chapwa za kupata maisha mazuri barani Ulaya. 

Makaburi kadhaa ya umati yamegunduliwa hivi karibuni huko Libya. Mwaka jana pia, miili mingine18 ilifukuliwa katika eneo la Sabaa katika mji wa pwani wa Sirte katikati ya Libya, ngome ya zamani ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS).

Kabla ya hapo pia, maafisa husika wa Libya walisema kuwa wamegundua miili 42 kwenye kaburi moja la umati katika eneo moja la shule katika mji wa Sirte.