Apr 20, 2024 02:57 UTC
  • Balozi wa Afrika Kusini mjini Doha: Kuitetea Palestina ni suala la kibinadamu

Balozi wa Afrika Kusini mjini Doha, Ghulam Hussein Asmal, amesema nchi yake ilifungua kesi ya kuitetea Palestina mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki dhidi ya utawala vamizi wa Israel unaoendelea kuua watu wa Ukanda wa Gaza tangu tarehe saba mwezi Oktoba mwaka jana kwa dhamira ya kutenda haki, akisisitiza kuwa hakuna sababu ya kuachana na kadhia hiyo.

Balozi Asmal amesisitiza ulazima wa kufanyika mageuzi katika Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama ili kutekeleza haki inayotakikana duniani. Amesema: "Haikubaliki kuwa na mataifa yaliyo juu ya sheria na mataifa mengine ambayo sheria ya kimataifa inatumika dhidi yao. Umoja wa Mataifa lazima utekeleze majukumu yake kwa umakini. Kuna ulazima wa kufanyika mageuzi makubwa ndani ya Baraza la Usalama na kutoruhusu nchi fulani kupewa ulinzi wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama na kutelekezwa nchi nyingine."

 Amefafanua kuwa nchi yake imeidhihirishia dunia kuwa suala la Palestina si suala la kidini wala si mzozo baina ya Waislamu na Mayahudi, kwani idadi ya Waislamu nchini mwake haizidi 2% ya watu wote, bali msingi wa suala hilo ni wa kibinadamu.

Balozi Ghulam Hussein Asmal

Balozi wa Afrika Kusini nchini Qatar pia ameeleza kuwa nchi yake inaunga mkono matakwa ya Palestina kupata uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa, akiashiria uhalali wa ombi hilo, na kwamba ni haki ya Wapalestina inayopaswa kuungwa mkono na nchi zote za dunia.

Vilevile ameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki kutekeleza majukumu yake kuhusu maamuzi ya mahakama hiyo dhidi ya Israel, na kufanya kazi ambayo iliundwa kwa ajili yake.