Rais Samia ataka ‘waliodumisha Muungano wa Tanzania waendelee kuenziwa'
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania waendelee kuwaenzi na kudumisha maono ya waasisi wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mwl. Julius Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume pamoja na viongozi waliofuatia baada yao, kutokana na juhudi zao za kuujenga na kuudumisha Muungano huo.
Rais wa Tanzania amesema hayo leo wakati akihutubia umati wa wananchi katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam wakati wa Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Nawatakia Watanzania wote kheri ya kutimiza miaka 60 ya Muungano wa Tanzania. Kwa niaba yenu Watanzania nawashukuru kwa dhati Waasisi wa Muungano Mwl. Nyerere na Mzee Karume pamoja na viongozi waliofuata baada yao kwa kutuleta pamoja na kujenga Taifa huru, madhubuti na lenye matumaini. Zawadi pekee tunayoweza kuwapa ni kuendelea kudumisha Muungano huu na kuyaenzi maono yao kwa msemo wa siku hizi tunasema, tuwape maua yao,” amesema Rais wa Tanzania.
Rais Samia amewashukuru wananchi kwa kujitokea kwa wingi katika shughuli hiyo ya shetehe ya Muungano licha ya mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya Tanzania na kusema: "Tumepata heshima ya kuungwa mkono na wakuu wa nchi na Serikali kutoka jumuiya ya SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki na wapo viongozi waliokuja kuwawakilisha marais wa nchi zao”.
Katika hotuba hiyo, Rais wa Tanzania amesema, katika kutekeleza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa mwaka 1964 Watanzania hawana budi kutekeleza kwa vitendo falsafa ya 4R.
Amesema: Haya ndiyo yatakayoendelea kujenga amani na utulivu wa kudumu nchini kwetu na kuleta maendeleo endelevu. Leo tuna fahari nchi imefika uchumi wa kati ngazi ya chini na kuna dalili za kuimarika ili kufikia uchumi wa ngazi ya juu."
Tangu aliposhika madaraka ya nchi, Machi 19 mwaka 2021, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akihubiri falsafa yake ya R nne (4R) anazozitumia katika utawala wake. 4R zina maana ya maridhiano, (reconciliation) mabadiliko (reforms), ustahamilivu (resilience) na kujenga upya (rebuilding).
Kwa upande wake, Rais wa Serikali ya Zanzibar ambaye pia amehutubia sherehe hiyo amesema, wakati taifa linasherehekea miaka 60 ya Muungano kuna hatua kubwa zimepigwa katika sekta za kiuchumi na huduma za kijamii. Dakta Hussein Mwinyi amesema Tanzania inaendelea kupata sifa kubwa kutokana na Muungano uliodumu na kuwa na amani, umoja na mshikamano.
Mwinyi amesema: Ni jambo la faraja na kutia moyo kuona mambo mengi yaliyoangaliwa kama changamoto za Muungano yameshapatiwa ufumbuzi, na machache yaliyobaki yapo katika hatua mbalimbnali kupatiwa ufumbuzi.
Sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zimehudhuriwa na marais wa nchi za Zambia, Kenya, Comoro, Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.