May 06, 2024 07:12 UTC
  •  OIC yataka Israel ibebeshwe dhima kwa jinai dhidi ya Wapalestina

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua na kuubebesha dhima utawala wa Kizayuni wa Israel, kutokana na jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo haramu dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Akihutubia mkutano wa 15 wa kilele wa OIC uliomalizika jana Jumapili katika mji mkuu wa Gambia, Banjul, Katibu Mkuu wa OIC, Hissein Brahim Taha amesema, jumuiya hiyo inaunga mkono jitihada za kutambuliwa taifa huru la Palestina, mji wake mkuu ukiwa Quds (Jerusalem), na nchi hiyo kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.

Taha ameeleza bayana kuwa, nchi zote wanachama wa jumuiya hiyo zimeafikiana kwa sauti moja juu ya kuunga mkono haki ya wakazi wa Gaza ya kufikishiwa misaada ya kibinadamu, na haki ya Wapalestina kuwa na taifa huru linalotambulika na UN.

Katibu Mkuu wa OIC amesisitizia haja ya kuwajibishwa Israel kwa vitendo vyake chini ya sheria za kimataifa, sanjari na kuunga mkono Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) ili liweze kuendelea na shughuli zake muhimu za kibinadamu huko Gaza.

Katibu Mkuu wa OIC, Hissein Brahim Taha

Kadhalika viongozi wa OIC waliohudhuria mkutano humo nchini Gambia wametaka kuwajibishwa na kubebeshwa dhima utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na jinai zake dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

Wamelaani vikali vita vinavyoendelea vya Israel katika Ukanda wa Gaza ambavyo vimepelekea Wapalestina karibu 35,000 kupoteza maisha, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.

Aidha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetoa wito wa kufanyika uchunguzi huru kuhusu jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Israel huko Gaza. Imetaja jinai hizo kuwa ni "uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu".

Tags