May 09, 2024 11:57 UTC
  • WFP: DRC inakabiliwa na 'janga la kibinadamu' kutokana na mafuriko

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuwa, eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo linakabiliwa na "janga la kibinadamu" baada ya kukumbwa na mafuriko makubwa yaliyoathiri takriban watu nusu milioni.

Kote karibu na Ziwa Tanganyika, na maeneo ya nyanda za juu za bonde la Mto Kongo, watu wamepoteza makazi yao, mashamba yao na maisha yao, ambapo WFP inakadiria watu 471,000 wameathirika na ekari milioni 1.1 zimefurika maji, zikiwemo hekta 21,000 za ardhi za mazao.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linaelezea wasiwasi wake kuhusu athari za utoaji wa huduma za afya huku magonjwa yakiathiri baadhi ya maeneo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa kuzingatia pia vurugu katika majimbo ya Kivu Kusini na Tanganyika shirika hilo limeyataja maeneo yaliathirika zaidi kuwa ni Haut-Lomami na Tanganyika ambayo inapakana nchi jirani za Burundi, Tanzania na Zambia.

 

Wakati huo huo, inaelezwa kuwa, maelfu ya wakimbizi katika nchi za Afrika Mashariki wamelazimika kuhama maeneo waliyokuwa wamepata hifadhi kufuatia  mvua kubwa ambazo zimesababisha mafuriko yaliyoambatana na maafa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limetaja wakimbizi walioathiriwa ni wale walioko Tanzania, Kenya, Somalia na Burundi.

Mafuriko katika nchi za Kenya na Tanzania yamepelekea watu wasiopungua 350 kufariki dunia na idadi hiyo inatazamiwa kuongezeka huku mvua zikilendelea kunyesha.