May 10, 2024 10:54 UTC
  • Seneti ya Nigeria yapendekeza hukumu ya kifo kwa ulanguzi wa dawa za kulevya

Baraza la Seneti la Nigeria limependekeza adhabu kali kwa ulanguzi wa dawa za kulevya, na kuifanya adhabu ya kifo kuwa hukumu mpya ya juu zaidi kupitia marekebisho ya sheria.

Marekebisho hayo ambayo bado hayajawa sheria, yanachukua nafasi ya kifungo cha maisha, ambacho hapo awali kilikuwa adhabu kali zaidi ya uhalifu wa ulanguzi wa dawa za kulevya.

Nigeria, nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika wanaokadiriwa kufikia zaidi ya watu milioni 200, katika miaka ya hivi karibuni imeondoka kutoka kuwa kituo cha kupitisha dawa za kulevya na kuwa mzalishaji kamili, mtumiaji na msambazaji dawa hizo.

Ingawa bangi inalimwa nchini Nigeria, dawa za kulevya kama kokeini, methamphetamine na mihadarati mingine huingizwa kwa njia za magendo kote nchini humo ili kushibisha tatizo linaloongezeka la uraibu wa dawa za kulevya katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika.

Waungaji mkono wa adhabu ya kifo kwa wahalifu wa ulanguzi wa dawa za kulevya wanasema kunyongwa kutatumika kama kizuizi kikubwa kwa walanguzi wa dawa za kulevya kuliko kifungo cha maisha jela.

Baraza la Seneti la Nigeria

Wabunge waliopinga muswada huo wameeleza wasiwasi wao kuhusu hali isiyoweza kutenduliwa ya adhabu ya kifo na uwezekano wa kutiwa hatiani kimakosa.