Zuma atoa onyo iwapo IEC itatangaza matokeo ya uchaguzi leo
(last modified Sun, 02 Jun 2024 06:38:57 GMT )
Jun 02, 2024 06:38 UTC
  • Zuma atoa onyo iwapo IEC itatangaza matokeo ya uchaguzi leo

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma ametishia kuchukua hatua ya kisheria ya kuizuia Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo (IEC) kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu leo Jumapili kama ilivyoratibiwa.

Zuma alitoa onyo hilo jana, baada ya chama chake cha Mkhonto weSizwe (MK) kutaka uchaguzi huo ufanyike upya, kikidai kuwa tayari kimewasilisha ithibati na vielelezo mbele ya IEC, vya kuonyesha kuwa uchaguzi huo umekubwa na kasoro nyingi.

Zuma amesema, "Tunahitaji muda, hakuna udharura wa kutangazwa (matokeo) kesho (leo Jumapili). Iwapo hilo litafayika, watachochea hisia zetu kwa kuwa tunafahamu wanachokifanya."

Vyama vingine vya upinzani vikiongozwa na Democratic Alliance (DA) vimesema ujumlishaji wa matokeo katika baadhi ya maeneo hasa katika mkoa wa Western Cape umekumbwa na mizingwe na uchakachuaji, na hivyo vinataka kura zihesabiwa upya.

Kwa mujibu wa asilimia 99.8 ya matokeo yaliyochapishwa kwenye tovuti ya Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini (IEC), chama tawala ANC kinaongoza kwa kuzoa takriban asilimia 40 ya kura, kikifuatiwa na chama cha Democratic Alliance (DA) kilichozoa asilimia 21.75, huku chama kipya cha Mkhonto weSizwe (MK) cha rais wa zamani, Jacob Zuma kikiambulia asilimia 14 ya kura.

Zuma (kushoto) akiwa na Rais Cyrill Ramaphosa walipokuwa wandani ANC

Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Julius Malema ambacho kilitazamiwa kutoa ushindani mkubwa dhidi ya chama tawala, kimezoa asilimia 9.54 ya kura. Kiongozi wake, Julius Malema tayari ametangaza masharti ya kuingia katika serikali ya mseto na ANC.

Licha ya kuwa kifua mbele, lakini chama cha ANC ambacho kimepoteza wingi wa viti bungeni kwa mara ya kwanza tangu 1994, kitalazimika kuingia katika muungano wa kitaifa na ama chama cha Democratic Alliance (DA), Economic Freedom Fighters (EFF), Mkhonto weSizwe (MK) au vyama vingine vidogo.