Jun 04, 2024 07:16 UTC
  • Umeme wazimwa, viwanja vya ndege vyafungwa Nigeria baada ya wafanyakazi kugoma

Shughuli muhimu zimesita nchini Ngeria baada ya umeme kukatika na viwanja vya ndege vikubwa kufungwa, kufuatia hatua ya vyama vikubwa zaidi vya wafanyakazi kuanzisha mgomo wa kudai nyongeza ya mishahara kutokana na ughali mkubwa wa maisha kuwahi kushuhudiwa nchini humo kwa miongo kadhaa.

Mgomo mpya ulianza jana Jumatatu baada ya kuvunjika mazungumzo ya kudai nyongeza ya kima cha chini cha mshahara yaliyofanyika kati ya serikali na mashirikisho makubwa mawili ya vyama vya wafanyakazi nchini humo vya Kongresi ya Wafanyakazi wa Nigeria (NLC) na Kongresi ya Muungano wa Wafanyakazi (TUC).

Vyama vya wafanyakazi vinataka kima cha chini cha sasa cha mshahara kwa mwezi cha dola 20 kiongezwe hadi karibu dola 336 huku Serikali ikiwa tayari kutoa dola 40.

"Tunadai ujira wa kuweza kuishi," umeeleza ujumbe uliowekwa na Kongresi ya Wafanyakazi ya Nigeria kwenye mtandao wa X, ikielezea kile wanachopata wafanyakazi kwa sasa kama "mshahara wa kubaki na njaa." Kongresi hiyo pamoja na Kongresi ya Muungano wa Wafanyakazi zinawakilisha mamia ya maelfu ya wafanyakazi wa serikali katika sekta muhimu.

Maandamano ya wafanyakazi

Mageuzi ya kiuchumi yaliyoletwa na Rais Bola Tinubu - ikiwa ni pamoja na kuondoa ruzuku ya mafuta - yamesababisha kupanda kwa mfumuko wa bei ambao uko katika rekodi ya juu zaidi katika kipindi cha miaka 28 iliyopita.

Katika mgomo huu wa sasa ulioanza jana Jumatatu, ambao ni wa nne tangu Tinubu aingie madarakani mwaka mmoja uliopita, wafanyakazi walifunga gridi ya taifa ya umeme na kuwafukuza waendeshaji katika kituo muhimu cha kusambaza umeme.

Hayo yameelezwa na Kampuni ya Ugavi wa Umeme ya Nigeria na kuongeza kuwa wafanyakazi wengine waliotumwa kurejesha umeme walizuiwa.

Kwingineko, wafanyakazi wa serikali ama waliamua kutofika kabisa maofisini au kufunga milango ya kuingilia, ikiwa ni pamoja na katika viwanja vya ndege katika mji mkuu Abuja na katika jiji la Lagos ambao ni kitovu cha shughuli za kiuchumi. Mamia ya abiria walikwama baada ya mashirika ya ndege ya eneo hilo kusimamisha shughuli za safari za ndege.../

Tags