Jun 06, 2024 04:24 UTC
  • Kadhaa waaga dunia baada ya mgodi wa dhahabu kuporomoka Nigeria

Makumi ya watu wanahofiwa kufariki dunia baada ya kuporomokewa na udongo kwenye mgodi wa dhahabu uliotelekezwa katikati ya Nigeria.

Hussaini Ibrahim, Msemaji wa Idara ya Dharura ya jimbo la Niger, katikati mwa Nigeria amesema kuwa, inakisiwa kuwa watu 30 wamenasa kwenye mgodi huo baada ya kuporomokewa na udongo.

Amesema, "Kufikia Jumatano hii, tunaamini kuwa watu 30 wangali wamefukiwa kwenye timbo. Hatuna idadi kamili kwa kuwa hata mashuhuda hawajui idadi ya watu waliokwama kwenye mgodi huo."

Hata hivyo afisa huyo wa serikali jimboni Niger amethibitisha kuwa mtu mmoja ameaga dunia kwenye mkasa huo wa kuporomokewa na udongo timboni. Mgodi huo uliporomoka Jumatatu iliyopita, baada ya mvua kubwa kunyesha katika eneo hilo.

Waziri wa Madini wa Nigeria, Dele Alake amesema maafisa kutoka Idara ya Uchimbaji Migodi wametumwa katika eneo la tukio katika kijiji cha Galadima Kogo kufuatilia mkasa huo kwa karibu.

Nchi ya Nigeria ambayo inapatikana magharibi mwa bara Afrika ina utajiri mkubwa wa madini kama vile dhahabu, almasi, na chuma. Hata hivyo shughuli za uchimbaji madini katika aghalabu ya matimbo ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika zinafanyika kinyume cha sheria na bila ya uangalizi wa vyombo vya dola.

Aghalabu ya madini hususan ya dhahabu yanayochimbwa kinyume cha sheria nchini humo pamoja na nchi nyingine za Afrika, husafirishwa kimagendo katika nchi za Ulaya na Uarabuni.

 

Tags