Jun 16, 2024 12:18 UTC
  • Ramaphosa kutangaza baraza la mawaziri jumuishi katika serikali ya umoja wa kitaifa

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, aliyechaguliwa tena kwa muhula wa pili baada ya chama chake cha ANC kudhoofika na kupoteza wingi katika bunge, anatarajiwa kutangaza baraza la mawaziri jumuishi.

Chama cha African National Congress (ANC) kimetangaza kuwa, Ramaphosa, ambaye ataongoza kile inachokiita serikali ya umoja wa kitaifa (GNU), atatangaza “baraza la mawaziri shirikishi GNU” baada ya uchaguzi mkuu wa Mei 29 kutotoa mshindi wa moja kwa moja.

Salamu za pongezi ziliendelea kumiminika kwa kiongozi huyo ambaye alichaguliwa tena kuwa rais siku ya Ijumaa na ataapishwa Juni 19.

Uchaguzi huo uliashiria mabadiliko ya kihistoria kwa Afrika Kusini, na kumaliza miongo mitatu ya utawala wa ANC wa hayati Nelson Mandela.

Chama cha ANC, ambacho kiliwahi kuongozwa na mwanasiasa wa kimataifa Nelson Mandela, kilitawala siasa za Afrika Kusini kwa miongo mitatu iliyopita hadi kilipopoteza wingi wake katika uchaguzi wa taifa na wa majimbo tarehe 29 Mei.

Chama hicho, ambacho kilikuwa kikipata zaidi ya 60% katika chaguzi zote tangu 1994, isipokuwa 2019, wakati ushindi wake ulipopungua hadi 57.5%, kilipata 40.18% tu ya kura katika uchaguzi wa mwaka huu. Hali hiyo imekiweka chama hicho katika wakati mgumu kuweza kuunda serikali peke yake.