Mamia ya askari polisi wa Kenya watumwa Haiti licha ya ukosoaji
Askari polisi 400 wa Kenya wameelekea nchini Haiti leo Jumanne kwa ajili ya kwenda kulinda usalama na kurejesha uthabiti katika nchi hiyo ya Caribbean.
Askari polisi hao wameondoka Nairobi, mji mkuu wa Kenya mapema leo Jumanne, siku moja baada ya Rais William Ruto wa nchi hiyo kuongoza hafla ya kuwaaga maafisa usalama hao, wanaoenda kuongoza kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa.
Akiongea katika hafla hiyo jana Jumatatu, Dakta Ruto alisema, "Ujumbe huu ni moja ya jumbe muhimu, wa dharura na wa kihistoria katika historia ya kuonyesha mshikamano na ulimwengu."
Taifa hilo la Afrika Mashariki linapanga kupeleka jumla ya maafisa 1,000 wa polisi kwa ajili ya operesheni hiyo. Kenya imekubali kuongoza kikosi hicho kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kulinda taifa hilo la Caribbean, licha ya pingamizi na ukosoaji wa vyama vya upinzani na asasi za kiraia.
Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la mwezi Oktoba mwaka jana liliidhinisha kupelekwa kwa kikosi hicho, lakini mahakama ya Kenya mwezi Januari mwaka huu ilichelewesha mchakato huo. Mahakama ilisema serikali haikuwa na mamlaka ya kupeleka maafisa wa polisi nje ya nchi bila ya kuwepo makubaliano ya awali.
Mbali na Kenya, nchi nyingine ambazo zilielezea nia ya kujiunga na kikosi hicho ni pamoja na Benin, Bahamas, Bangladesh, Barbados na Chad. Ghasia za magenge ziliikumba Haiti miaka mingi iliyopita, lakini ziliongezeka zaidi tangu kuuawa Rais Jovenel Moise mnamo 2021.
Umoja wa Mataifa unakadiria mzozo huo ulisababisha vifo vya takriban watu 5,000 mwaka jana na kupelekea wengine 300,000 kuhama makazi yao, huku kukiwa na uhaba wa chakula na huduma za matibabu.