Jun 25, 2024 13:40 UTC
  • Julian Assange
    Julian Assange

Mwanzilishi wa tovuti ya kufichua kashfa mbalimbali, "WikiLeaks", Julian Assange, ameachiwa huru kutoka jela nchini Uingereza baada ya kufungwa kwa miaka 14.

Tovuti ya Wikileas, iliyovujisha taarifa na nyaraka za siri za uhalifu wa kijeshi wa Marekani nchini Iraq na Afghanistan, imechapisha ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X na kutangaza kuwa, Julian Assange ameachiliwa huru kutoka jela ya Belmarsh mjini London leo Jumanne baada ya kufungo cha miaka 14 na ameondoka Uingereza kuelekea kwenye makazi yake, nchini Australia.

Kuachiwa huru Assange kumefanyika baada ya makubaliano na mfumo wa mahakama wa Marekani, ambapo kwa mujibu wake, Assange alitakikana kukiri kwamba alikiuka Sheria ya Ujasusi ya Marekani.

Katika kipindi chote cha karibu muongo mmoja wa kazi zake, WikiLeaks imevujisha zaidi ya nyaraka 700,000 za siri kijeshi. Nyaraka hizi zilifichua uhalifu na jinai za serikali ya Marekani nchini Iraq na Afghanistan, ikiwa ni pamoja na mauaji raia wa Iraq kwa kutumia helikopta za kijeshi za Marekani na mateso ya mahabusi kwenye jela ya Guantanamo.

Nyaraka zilizofichuliwa na Assange kuhusu vita vya Iraq zinaonyesha kuwa, raia 66,000 wa nchi hiyo waliuawa na vikosi vya jeshi la Marekani au kuteswa magerezani.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu duniani yamekuwa yakitoa wito wa kuachiwa huru Assange kwa miaka mingi.

Kufungwa kwa kipindi cha miaka 14 mwanzilishi huyo wa WikiLeaks kuliweka wazi uongo wa madai ya nchi za Magharibi eti ya kutetea uhuru wa kusema na upashaji huru wa habari.