Jun 24, 2024 03:29 UTC
  • Kushadidi mivutano ya kijeshi baina ya Russia na Marekani

Mvutano wa kijeshi na kiusalama kati ya Russia na Marekani umeongezeka kutokana na hatua za kiuhasama za Washington dhidi ya Moscow, hasa baada ya Washington kuiruhusu Ukraine kushambulia ardhi ya Russia kwa kutumia silaha za Marekani.

Wakati huo huo, Russia inakusudia kuimarisha zaidi vikosi vyake vya kimkakati vya nyuklia ili kukabiliana na ongezeka la misimamo ya uhasama ya shirika la NATO linaloongozwa na Marekani.

Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imetangaza kuwa, jeshi la Ukraine linaruhusiwa kutumia makombora ya masafa marefu ya Marekani kushambulia maeneo ya ardhi ya Russia. Msemaji wa Pentagon, Patrick Ryder, alidai kuwa Russia inatumia ardhi yake kama "eneo salama" na kushambulia maeneo ya Ukraine kutoka ndani ya mipaka yake. Aliongeza kuwa: "Kwa kuwa tumeshuhudia operesheni kama hii ya vikosi vya Russia, tumeitangazia Ukraine kwamba inaweza na ina haki ya kujibu mashambulizi haya kwa ajili ya kujilinda." Hata hivyo, Pentagon ilidai kuwa idhini hii haina maana ya kupitishwa sera mpya. 

Patrick Ryder

Maafisa wa Ukraine wametangaza kuwa, Marekani imebana matumizi ya silaha hizo kulenga shabaha umbali wa chini ya kilomita 100 kutoka mpakani. Maafisa wa serikali ya Marekani wamekataa kuthibitisha habari hii. Wakati huo huo, Ikulu ya Rais wa Marekani ilitangaza Alhamisi iliyopita kuwa, inapanga kuharakisha mpango wa kupeleka mifumo ya ulinzi wa anga huko Ukraine. Hapo awali Marekani iliipatia Ukraine mifumo ya ulinzi wa anga, ikiwa ni pamoja na Patriot na mfumo wa kujikinga na makombora wa NASAMS.

Vitendo vya uchochezi na vya kichokozi vya Washington dhidi ya Moscow kwa kutoa idhini kwa Kiev kushambulia ardhi ya Russia kwa makombora ya Marekani vinafanyika ili kuidhoofisha nchi hiyo kadiri iwezekanavyo, haswa katika suala la kijeshi, na pia kusababisha uharibifu mkubwa zaidi kwa miundombinu ya kijeshi na viwanda vya Russia katika maeneo ya mbali. Marekani na NATO, ambazo zimetuma zaidi ya dola bilioni mia moja za msaada wa kijeshi na silaha kwa Ukraine, bado zinataka kuendeleza vita vya umwagaji damu nchini Ukraine kwa lengo la kuidhoofisha Russia kadiri inavyowezekana.

Wakati huo huo, NATO pia imezidisha sera zake za kivita dhidi ya Russia. Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, ameeleza kwamba muungano huo wa kijeshi wa Magharibi unapingana na Russia na China, na kutangaza kwamba wanachama wa NATO wameanza harakati za maandalizi ya kukabiliana na silaha za nyuklia. Katika suala hili, NATO inafanya mazungumzo na nchi wanachama ili kuweka tayari vichwa vya silaha za nyuklia kwa ajili ya uwezekano wa kukabiliana na Russia na China. Stoltenberg alidai kuwa vitisho vya China na Russia vimeongezeka. 

Jens Stoltenberg

Maafisa wakuu wa Marekani na shirika la NATO wanaamini kwamba, ushindi wa Russia katika vita vya Ukraine, utakuwa na maana ya kudharauliwa na kudunishwa shirika hilo la kijeshi na kupanuka ushawishi na nguvu za kikanda na kimataifa za Russia, jambo ambalo litabadilisha mahesabu ya kiusalama, kijeshi na kisiasa barani Ulaya kwa madhara ya nchi za Magharibi. Aidha, Washington inaona vita vya Ukraine kuwa ni fursa muhimu ya kudhoofisha uwezo wa kijeshi wa Russia kadiri inavyowezekana. Hata hivyo, inatupasa kusema kuwa, kuendelea vita hivi kuna maana ya hasara zaidi na zaidi za mauaji ya binadamu na uharibifu wa nyenzo kwa Russia na Ukraine, na hatimaye kusambaratika Ukraine kama nchi kubwa ya Ulaya, kwa ajili ya malengo ya Marekani.

Wakati huo huo, Russia imejibu hujuma za NATO na Marekani. Katika hatua ya karibuni zaidi ya Moscow, Rais Vladimir Putin alitangaza siku ya Ijumaa kwamba ana mpango wa kutengeneza silaha tatu za nyuklia, ambazo ni pamoja na ndege za kivita za kistratijia, nyambizi zenye uwezo wa kubeba silaha za nyuklia na makombora ya balestiki ya bara hadi bara jingine. 

Nyambizii ya kijeshi ya Russia

Kwa hakika, Russia ambayo kwa sasa inakabiliana na hatua za kichokozi za NATO na Marekani katika muundo wa msaada mkubwa wa kijeshi kwa Ukraine, misaada ya kijasusi na kutumwa vikosi vya nchi za Magharibi kuisaidia Ukraine, tahadhari ya nyuklia ya NATO, na sasa hatua ya Washington ya kuiruhusu Ukraine kutumia silaha Wamarekani dhidi ya ardhi ya Russia na kadhalika, haina chaguo ila kuongeza mkakati wake wa kuzalisha silaha za nyuklia kama jibu la kushadidi uadui wa Magharibi, na dhamana ya kudumisha usalama wake wa kitaifa.

Kwa utaratibu huo tunaona kuwa, mvutano kati ya Russia na Marekani unaongezeka kila uchao, na kuendelea kwake kunaibua hatari nyingi kwa usalama wa Ulaya na baadaye, usalama wa kimataifa.

Tags