UN yataka kuanza mazungumzo ya kitaifa Kongo
Mkuu wa kikosi cha kimataifa cha kulinda amani katika Jamhuri yqa Kidemokrasia ya Kongo ametilia mkazo udharura wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa kwa ajili ya kuzuia kushadidi mgogoro nchini humo.
Maman Sidikou amesema jamii ya kimataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutokea ghasia na machafuko ya kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Uchaguzi huo umepangwa kufanyika mwezi Disemba mwaka huu.
Mkuu wa kikosi cha askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo amesema kuwa, mazungumzo yatakayoshirikisha makundi yote baina ya serikali ya Kongo na kambi ya upinzani ndiyo yanayoweza kukomesha mivutano iliyopo hivi sasa nchini humo.
Mwaka jana Rais Joseph Kabila wa Kongo akitoa wito wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa kwa ajili ya kudhamini uchaguzi huru na wa haki lakini wapinzani wa serikali wamekataa wito huo wakisema ni jaribio la kiongozi huyo la kutaka kung'ang'ania madaraka baada ya kumalizika kipindi cha uongozi wake.