Benki ya ADB kuipa msaada wa fedha Sudan Kusini
Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) imetangaza habari ya kuipa Sudan Kusini msaada wa fedha ili itatuwe matatizo yake ya maji.
Benki hiyo ilitangaza jana (Jumamosi) kuwa, imefikia uamuzi wa kuipa Sudan Kusini msaada wa dola milioni 6 na nusu kwa ajili ya kuendeshea mradi wa kusambaza maji safi mjini Juba.
Kwa mujibu wa benki hiyo, mradi huo utakapokamilika utawafaidisha watu laki mbili na 30 elfu wa mjini Juba.
Imeongeza kuwa, shabaha ya kutolewa msaada huo ni kunyanyua kiwango cha maisha ya wakazi wa Juba kupitia kuimarisha miundombinu ya mji huo yakiwemo maji safi ya kunywa.
Tamko hilo la Benki ya Maendeleo ya Afrika limetolewa katika hali ambayo hali bado ni tete katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, kutokana na machafuko ya hivi karibuni baina ya wafuasi wa Rais Salva Kiir na wale wa makamu wake, Riek Machar.
Mapigano hayo yamepelekea zaidi ya watu 300 kuuawa na maelfu ya wengine kuyakimbia makazi yao. Baadhi ya duru za habari zinasema idadi ya waliouawa katika mapigano hayo yaliyoanza siku ya Alkhamisi iliyopita imepindukia watu 1,000.
Nchi mbalimbali zikiwemo za Afrika na Ulaya zimeondoa raia wao mjini Juba kutokana na machafuko hayo.