Jul 27, 2024 07:02 UTC
  • Mvua kubwa yazidisha mateso ya wakimbizi mashariki mwa Sudan

Mvua kubwa inayoendelea kunyesha huko mashariki mwa Sudan imezidisha mateso ya watu waliokimbia makazi yao haswa katika miji ya Gedaref, Kassala na Halfa Aj Jadeedah.

Ripoti zinasema maji ya mvua kubwa iliyonyesha jana Ijumaa yamejaa katika mitaa na mji wa Kassala na kusuababisha matatizo makubwa kwa wakazi wa eneo hilo.

Watu walioshuhudia wamesema kuwa maji ya mvua yalifurika kwenye makazi ya watu na kuzingira mahema ya wakimbizi.

Idara ya Masuala ya Dharura ya Kassala imeonya kuhusu hali mbaya katika baadhi ya makazi ya watu, na kutoa wito kwa serikali na mashirika yote ya kimataifa kuwasaidia wakimbizi wa eneo hilo, na kuwasilisha misaada ya nguo za watoto na vifaa vya kupasha joto.

Hali kama hiyo ya mafuriko na mvua kubwa zilizowaathiri wakimbizi pia imeshuhudiwa katika miji ya Gedaref na Halfa Aj Jadeedah.

Zaidi ya Wasudani milioni kumi wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe. 

Mvua kubwa iliyonyesha katika nchi jirani ya Ethiopia pia imesababisha maporomoko ya udongo katika eneo la Gofa na ripoti zinasema zaidi ya watu 250 wameaga dunia kutokana na janga hilo la kimaumbile. 

Tags