Mfalme wa Morocco aweka wazi azma ya nchi hiyo kurejea AU
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11470-mfalme_wa_morocco_aweka_wazi_azma_ya_nchi_hiyo_kurejea_au
Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco ametangaza wazi azma ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ya kutaka kurejea katika Umoja wa Afrika AU, baada ya kuondoka katika umoja huo zaidi ya miongo mitatu iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 18, 2016 03:09 UTC
  • Mfalme wa Morocco aweka wazi azma ya nchi hiyo kurejea AU

Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco ametangaza wazi azma ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ya kutaka kurejea katika Umoja wa Afrika AU, baada ya kuondoka katika umoja huo zaidi ya miongo mitatu iliyopita.

Mfalme huyo amewatumia ujumbe viongozi wa Kiafrika wanaoshiriki mkutano wa Umoja wa Afrika ulioanza rasmi jana huko Kigali, mji mkuu wa Rwanda na kusema wakati umefika kwa nchi hiyo ya Kiarabu kurejea katika nafasi yake kwenye umoja huo. Mfalme Mohammed VI wa Morocco amewaambia viongozi wa AU katika ujumbe huo kuwa, ingawaje Morocco iliondoka AU, lakini haikuondoka barani Afrika. Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Salahuddine Mezouar hivi karibuni amekuwa katika safari za kidiplomasia katika nchi kadhaa za Kiafrika zikiwemo Misri, Libya, Sudan, Senegal, Tunisia, Cameroon, Cote D'ivoire na Ethiopia ili kuzitaarifu kuhusu uamuzi huo wa Rabat. Ikumbukwe kuwa, mwaka 1984, Morocco kupitia Mfalme Hassan II, babake mfalme wa sasa, iliamua kujiondoa katika umoja huo wakati huo ukifahamika kama Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU), kufuatia uamuzi wa umoja huo wa kuafiki uanachama wa Jamhuri ya Sahara Magharibi iliyojitangaza kuwa huru, licha ya serikali ya Rabat kuihesabu kuwa sehemu ya ardhi yake.