Wanaigeria warejea mitaani licha ya ombi la Rais
Wananchi katika mji wa Lagos, Nigeria jana walimiminika mitaani kuendelea na maandamano yao ya kupinga hali mbaya ya uchumi licha ya ombi la Rais wa nchi hiyo Bola Tinubu la kusitishwa maandamano.
Maandamano hayo ya wananchi wa Nigeria chini ya anwani "siku za ghadhabu", yanapinga kupanda pakubwa kwa gharama ya maisha nchini humo. Waandamanaji wanalalamikia pia uendeshaji mbaya wa nchi na ufisadi katika nchi hiyo ya Kiafrika yenye idadi kubwa ya watu na mzalishaji mkubwa wa mafuta.
Waandamanaji wanasema kuwa wamevutiwa na kutiwa moyo na vijana nchini Kenya ambao mwezi uliopita waliitisha maandamano wakipinga ongezeko la kodi.
Maandamano yote mawili ya Nigeria na huko Kenya yanalalamikia serikali za nchi hizo kwa kushindwa kutimiza ahadi zao zilizowaingiza madarakani. Akihutubia taifa Rais Bola Tinubu wa Nigeria ametetea mageuzi aliyoyataja kuwa ya kishujaa ambayo yalipasa kunusuru fedha za serikali.