Jeshi la Sudan lathibitisha kuzima shambulizi la RSF huko El Fasher
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115096-jeshi_la_sudan_lathibitisha_kuzima_shambulizi_la_rsf_huko_el_fasher
Jeshi la Sudan limetangaza kuwa limezima shambulio la Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kwenye mji wa El Fasher, makao makuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, baada ya saa kadhaa za mapigano makali kati ya pande hizo mbili.
(last modified 2024-08-11T07:37:18+00:00 )
Aug 11, 2024 07:37 UTC
  • Jeshi la Sudan lathibitisha kuzima shambulizi la RSF huko El Fasher

Jeshi la Sudan limetangaza kuwa limezima shambulio la Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kwenye mji wa El Fasher, makao makuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, baada ya saa kadhaa za mapigano makali kati ya pande hizo mbili.

Vyanzo vya ndani vimeripoti kwamba jana, Jumamosi, Al Fasher ilishuhudia mapigano ambayo yametambuliwa kuwa makali zaidi ambayo yaliendelea kwa saa 9. Mapigano hayo yalifuatia shambulizi la Vikosi vya Msaada wa Haraka kwenye mji huo kutokea pande 3. Jeshi la Sudan limetangza kuwa limefanikiwa kuzima shambulizi hilo.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Jeshi la Sudan, Brigedia Jenerali Nabil Abdullah, imesema: "Vikosi vyetu vimesambaratisha shambulio kubwa la wanamgambo magaidi wa Dagalo katika mji wa El-Fasher."

Kwa upande wake, Harakati ya Ukombozi wa Sudan, ambayo linapigana pamoja na jeshi, imeripoti kwamba Vikosi vya Msaada wa Haraka vilijaribu kuvamia mji wa El Fasher kutokea pande zote baada ya kukusanya maelfu ya wapiganaji.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Vikosi vyetu vimetoa funzo la vita kwa RSF, kwa kuua mamia ya wapiganaji wa kundi hilo na kusambaratisha washambuliaji."

Gavana wa eneo la Darfur, Minni Arko Minawi, pia amesema kuwa vikosi vya pamoja vilivyoshirikiana na jeshi la Sudan jana vilisambaratisha wapiganaji wa RSF katika mji wa El Fasher.

Siku kadhaa zilizopita, Muungano wa Madaktari nchini Sudan ulisema kuwa, mji wa El Fasher, makao makuu ya Jimbo la Darfur Kaskazini la magharibi mwa nchi hiyo umegeuka na kuwa mahali hatari na pabaya zaidi kuishi binadamu duniani kutokana na vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi.