Viongozi wakuu wa upinzani Tanzania watiwa mbaroni
Polisi ya Tanzania imemkamata mwanasiasa kigogo wa chama kikuu cha upinzani cha demokrasia na maendeleo, CHADEMA, Tundu Lissu, pamoja na viongozi wengine wa chama hicho Jumapili jioni.
Taarifa hizo zimetolewa na mkuu wa mawasiliano wa CHADEMA, John Mrema, kupitia ujumbe katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa X. Amesema Lissu na viongozi wengine walikamatwa mkoani Mbeya ambako walikwenda kushiriki mkutano wa kuadhimisha siku ya vijana duniani uliopangwa kufanyika leo Jumatatu.
Mkutano huo uliandaliwa na tawi la vijana la CHADEMAlakini Polisi ilitangaza kuuzuia kwa madai ya kuwepo mipango ya kufanyika maandamano ya vurugu.
Kiongozi wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amelaani kukamatwa kwa Lissu na viongozi wengine waandamizi pamoja na wanachama na kuitaka polisi kuwaachia huru bila masharti yoyote.
Awadh Haji, mkuu wa polisi anayehusika na operesheni na mafunzo, alisema jeshi la polisi “limeona ishara za wazi kwamba lengo lao sio kuadhimisha siku ya kimataifa ya vijana bali kuanzisha na kushiriki katika vurugu.”
Taarifa yake ilitoa mfano wa vijana wa Kenya, ikionekana kumaanisha wiki kadhaa za maandamano ya kuipinga serikali katika nchi jirani ya Afrika Mashariki yaliyoongozwa kwa kiasi kikubwa na vijana.
“Polisi waliamua kupiga marufuku mkutano wa aina yoyote wa ndani na wahadhara au maandamano ambayo yamepangwa kufanyika chini ya jina la kuadhimisha siku ya vijana,” Haji alisema, akionya kuwa yanaweza kusababisha kuvurugika kwa amani.
Maafisa wa chadema wamelaani uamuzi huo, na kumtaka Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati, wakiituhumu polisi kwa kujaribu kuzuia misafara ya magari inayoelekea Mbeya na kuwakamata baadhi ya vijana.