Mtuhumiwa mkuu wa mauaji ya Shakahola akana mashtaka ya mauaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115168-mtuhumiwa_mkuu_wa_mauaji_ya_shakahola_akana_mashtaka_ya_mauaji
Paul McKenzie, kiongozi wa kanisa la kufunga hadi kufa nchini Kenya amekana mashtaka ya mauaji ya kutokusudia kufuatia vifo vya waumini zaidi ya 400 katika mkasa unaohusiana na ibada katika pwani ya Kenya.
(last modified 2024-08-12T23:08:01+00:00 )
Aug 12, 2024 23:08 UTC
  • Mtuhumiwa mkuu wa mauaji ya Shakahola akana mashtaka ya mauaji

Paul McKenzie, kiongozi wa kanisa la kufunga hadi kufa nchini Kenya amekana mashtaka ya mauaji ya kutokusudia kufuatia vifo vya waumini zaidi ya 400 katika mkasa unaohusiana na ibada katika pwani ya Kenya.

McKenzie pamoja na washukiwa wengine 94, walifikishwa mahakamani mjini Mombasa jana Jumatatu na kukanusha mashtaka.

Kasisi huyo na washtakiwa wenzake wanakabiliwa na mashtaka mengi ya kuua bila kukusudia katika mauaji ambayo yamepatiwa jina la mauaji ya Shakahola.

McKenzie ambaye alikamatwa Aprili iliyopita, baada ya miili kugunduliwa katika Msitu wa Shakahola, anatuhumiwa kuwahimiza wafuasi wake wafe kwa njaa ili "kumlaki Yesu," habari iliozua mshtuko mkubwa nchini Kenya na kote duniani.

Mwendesha mashtaka Alexander Jami Yamina amesema kuwa, kesi hiyo ni ya kipekee nchini Kenya, na washukiwa watashtakiwa chini ya sheria inayohusiana na makubaliano ya kujitoa uhai.

Maiti zikikusanywa katika eneo la Shakahola

 

Takriban mashahidi 420 wameandaliwa na upande wa mashtaka huku kesi hiyo ikipangwa kuendelea kwa siku nne hadi Alhamisi.

Mwezi Machi mwaka huu, mamlaka ilianza kutoa miili ya baadhi ya waathiriwa kwa ndugu zao baada ya miezi kadhaa ya kazi kubwa ya kuwatambua kwa kutumia chembechembe za DNA. Hadi sasa milii 34 imerejeshwa.

Mackenzie alikuwa ameanzisha Kanisa lake la Good News International Church mwaka wa 2003, lakini akasema alilifunga mwaka wa 2019 na kuhamia Shakahola kujiandaa na kile alichotabiri kuwa mwisho wa dunia Agosti mwaka jana.