Polisi Tanzania yawaachia kwa dhamana baadhi ya viongozi wa Chadema, wengine wakwama
Jeshi la Polisi katika mkoa wa Mbeya nchini Tanzania limethibitisha kuwashikilia na kuwahoji viongozi na wafuasi wapatao 520 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuwaachia huru baadhi yao kwa dhamana.
Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo imesema, ambao hawajaachiwa, ni wale ambao wameshindwa kukidhi masharti ya dhamana au kuwa na makosa zaidi ya moja, likiwemo la jinai.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa jeshi la polisi halitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka sheria na taratibu za nchi kwa kuiga mataifa mengine.
Akitoa taarifa hiyo usiku wa kuamkia leo, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi la Tanzania Awadhi Haji amesema, Jumapili Agosti 11 walikamatwa watu 375, wakiwemo wanaume 261 na wanawake 114 na kwamba jana Jumatatu, jeshi hilo liliwatia mbaroni watu 145, wakiwemo wanaume 112 na wanawake 33.
Akifafanua zaidi, Kamishna Haji amesema: "Agosti 12 Jeshi la Polisi limewakamata wafuasi wengine 145 wakiwamo viongozi wakuu wa chama hicho Taifa, ambao ni Mwenyekiti Freeman Mbowe na Mwenyekiti Bavicha Taifa John Pambalu katika uwanja wa ndege Songwe wakija kushiriki kongamano lililopigwa marufuku".
Kamanda huyo wa polisi amewataka viongozi wote wa vyama vya siasa na wafuasi wao kufuata sheria na taratibu za nchi na kuonya kuwa jeshi hilo litachukua hatua kali za kisheria kwa mtu au kikundi kitakachojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani.../