Mazungumzo ya Sudan na Marekani yasambaratika Jeddah, matumaini ya amani yapotea
Sudan imetangaza kufeli mazungumzo yake na ujumbe wa Marekani mjini Jeddah, Saudi Arabia, suala ambalo linazidi kupoteza matumaini ya kupatikana amani nchini Sudan katika siku za hivi karibuni.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, hivi karibuni Marekani ililiomba Jeshi la Sudan (SAF) chini ya Jenerali Abdel Fattah al Burhan na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vinavyoongozwa na Jenerali Mohammad Hamdan Dagalo kufanya mazungumzo na ujumbe wake huko Jeddah Saudi Arabia kabla ya mazungumzo ya nchini Uswisi lakini kwanza kundi la RSF lilikataa ombi hilo la Marekani na pili Jeshi la Sudan lililoshiriki kikao hicho limesema mazungumzo yao na Wamarekani yamefeli.
Mkutano wa Geneva Uswisi kuhusu mgogoro wa Sudan, utafanyika chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Misri na Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) lakini tangu hivi sasa imekuwa ni vigumu kutabiri kufanikiwa mkutano huo kukomesha vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi nchini Sudan.
Siku ya Ijumaa, Jeshi la Sudan (SAF) lilipeleka wajumbe wake mjini Jeddah kwenda kuzungumza na ujumbe wa Marekani kuhusu ajenda ya mkutano wa Geneva lakini Jeshi la Sudan limetoa taarifa na kutangaza kuwa, mazungumzo ya wajumbe wake huko Jeddah hayakuendelea kwani hakuna kitu kipya kilichowasilishwa na ujumbe wa Marekani.
Baraza la Uongozi la Sudan chini ya jeshi la nchi hiyo limesema katika taarifa yake kuwa wajumbe wake wamegundua katika mazungumzo ya Jeddah kwamba Marekani haiamini kuwa ni wajibu wake kulilazimisha kundi la RSF kutekeleza haraka Mkataba wa Jeddah hivyo haukuona haja ya kuendelea na mazungumzo na Marekani.