Aug 14, 2024 04:21 UTC
  • Afrika yatangaza 'dharura ya afya ya umma' ya Homa ya Mpox

Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika kimetangaza "dharura ya afya ya umma", kiwango chake cha juu zaidi cha tahadhari, juu ya mlipuko wa Mpox unaokua katika bara hilo, na kutoa "wito wa wazi wa kuchukua hatua" kukomesha kuenea kwake.

Jumla ya visa 38,465 vya ugonjwa huu, ambao zamani ulijulikana kama Homa ya nyani, vimerekodiwa katika nchi 16 za Afrika tangu mwezi Januari 2022, pamoja na vifo 1,456, na ongezeko la 160% la kesi mnamo mwaka 2024 ikilinganishwa na mwaka uliopita, kulingana na data zilizochapishwa wiki iliyopita na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika, Africa CDC.

"Mlipuko wa Mpox sasa umevuka mipaka, na kuathiri maelfu ya watu katika bara letu (...) Ninaamua kusema, kwa moyo mzito lakini kwa dhamira isiyotetereka kwa raia wetu, kwa raia wetu wa Kiafrika, kwamba tunatangaza mlipuko wa Mpox kama dharura ya afya ya jamii barani Afrika." amesema Mwenyekiti wa Africa CDC, Jean Kasenya, wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Mama akiwa na mwanawe aliyeambukizwa homa ya MPOX

 

Ripoti zinaonyesha kuwa spishi hiyo ya Mpox inaambukiza kwa wingi na hivyo kupelekea kusambaa kwa haraka baina ya watu, na kusababisha wasiwasi mkubwa kwa wataalamu wa WHO.

Kulingana na CDC ya Afrika, karibu 70% ya kesi nchini Kongo DR zinahusu watoto wenye umri wa miaka 15 na chini, na watoto hao ni 85% ya vifo vilivyotokea.

Kesi za Mpox ziliripotiwa kwa mara ya kwanza wiki iliyopita katika nchi za Burundi na Rwanda, huku kesi zaidi zikigunduliwa pia nchini Kenya na Jamhuri ya Afrika ya Kati.