Algeria yataka kutekelezwa azimio la Baraza la Usalama la kusitisha vita Gaza
Balozi na mwakilishi wa Algeria katika Umoja wa Mataifa amelaani shambulio la Israel dhidi ya shule ya Tabeen huko Gaza na kutaka kutekelezwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kusimamisha vita huko Gaza.
Ammar bin Jame amesema hayo kwenye kikao cha Baraza la Usalama kuhusu Gaza na mashambulizi ya Israel katika shule ya Tabeen na kuongeza kuwa, Israel inakataa kutekeleza azimio la baraza hilo kuhusu usitishaji vita mara moja katika Ukanda wa Gaza.
Balozi wa Algeria katika Umoja wa Mataifa amesisitiza: Kwa mara nyingine tena tunatangaza kuunga mkono juhudi za upatanishi za Misri, Qatar na Marekani kufanikisha usitishaji vita huko Gaza. Azimio la Baraza la Usalama la kusitisha mapigano Gaza lazima litekelezwe mara moja. Lakini vikosi vinavyoikalia kwa mabavu vya Israel vilikaidi azimio hili la kusitisha mapigano huko Gaza.
Kadhalika Ammar bin Jame amesema: Jukumu la Baraza la Usalama ni kushughulikia sababu kuu ya kadhia ya Palestina ambayo ni kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina.
Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ambao umekhalifu kutekeleza azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililoamuru kusitishwa mapigano mara moja, unakabiliwa na shutuma za kimataifa kutokana na kuendeleza mashambulizi ya kikatili dhidi ya Ghaza tangu ilipotekelezwa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa na harakati ya Hamas Oktoba 7, 2023.
Huku zaidi ya miezi 10 ikiwa imepita tokea yalipoanza mashambulizi hayo ya Israel, maeneo mengi ya Ghaza yamegeuka magofu huku Israel ikiendelea kuweka vizuizi vikali dhidi ya uingizaji chakula, maji safi na dawa katika eneo hilo.