Polisi Kenya watuhumiwa; Walikuwa wakijua uhalifu uliofanyika Shakahola, asema shahidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115280-polisi_kenya_watuhumiwa_walikuwa_wakijua_uhalifu_uliofanyika_shakahola_asema_shahidi
Maafisa usalama walikuwa na nafasi ya kuepusha maafa ya vivyo vya zaidi ya watu 400 Shakahola iwapo wangefuatilia kwa undani ripoti za uvamizi wa eneo hilo mwaka wa 2021.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Aug 16, 2024 04:02 UTC
  • Polisi Kenya watuhumiwa; Walikuwa wakijua uhalifu uliofanyika Shakahola, asema shahidi

Maafisa usalama walikuwa na nafasi ya kuepusha maafa ya vivyo vya zaidi ya watu 400 Shakahola iwapo wangefuatilia kwa undani ripoti za uvamizi wa eneo hilo mwaka wa 2021.

Hayo ni kwa mujibu wa shahidi katika kesi inayomkabili Paul McKenzie, kiongozi wa Kanisa la Good News International Church ambaye yeye na wenzake wanatuhumiwa kusababisha vifo vya mamia ya watu kwa kuwaamuru wajizuiye kula chakula hadi wafe kwa njaa ili waweze kukutana na Yesu Kristo huko mbinguni.

Vyombo vya habari vya Kenya vimeripoti kuwa, imebainika mahakamani kuwa, dalili za mapema zilizoonyesha kuwa shughuli haramu zilikuwa zikiendelea ndani ya Msitu wa Shakahola mapema mwaka wa 2021, zilipuuzwa na kupelekea watu zaidi ya 429 kupoteza maisha yao katika eneo hilo miaka miwili baadaye.

Aliyekuwa afisa mkuu wa kituo cha polisi cha Lango Baya (OCS), Inspekta Hamara Hassan, amekiri mbele ya Mahakama ya Mombasa kwamba ripoti ya uvamizi, ugavi na uuzaji wa ardhi kiharamu iliripotiwa katika kituo chao mnamo Agosti 4, 2021, lakini kesi hiyo haikufuatiliwa zaidi na vyombo vya usalama ili kubaini waliohusika.

Mapema mwaka huu, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma nchini Kenya, (ODPP) ilitangaza kwamba imefanikiwa kupata ushahidi wa kutosha wa kuwashtaki washukiwa 95 wa mauaji ya Shakahola katika kaunti ya Kilifi eneo la pwani.

Paul McKenzie na wenzake

Mackenzie na wafuasi wake kadhaa walikamatwa mwaka jana mwezi Aprili na wamekuwa kizuizini tangu wakati huo ili kutoa nafasi kwa uchunguzi.

Miili ya watu 429 wakiwemo watoto imefukuliwa kutoka maeneo ya makaburi huko Shakahola na uchunguzi umebaini kuwa mbali na kufa njaa  wengine wakibainika kupoteza maisha kwa kunyongwa.