UNICEF yaonya kuhusu hali mbaya ya watoto nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115312-unicef_yaonya_kuhusu_hali_mbaya_ya_watoto_nchini_sudan
Watoto nchini Sudan wanateseka kwa hali mbaya inayozidi kuwa hatarishi huku vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi vikiendelea bila ya kuonesha dalili za kupungua. Mbali na hayo, mgogoro wa hali ya hewa nao unaweza kusababisha makumi ya maelfu ya vifo vya watoto katika miezi ijayo huko Sudan.
(last modified 2024-08-17T00:54:53+00:00 )
Aug 17, 2024 00:54 UTC
  • UNICEF yaonya kuhusu hali mbaya ya watoto nchini Sudan

Watoto nchini Sudan wanateseka kwa hali mbaya inayozidi kuwa hatarishi huku vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi vikiendelea bila ya kuonesha dalili za kupungua. Mbali na hayo, mgogoro wa hali ya hewa nao unaweza kusababisha makumi ya maelfu ya vifo vya watoto katika miezi ijayo huko Sudan.

Onyo hilo limetolewa na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF) kupitia msemaji wake James Elder ambaye ameliambia shirika la habari la Anadolu akiwa nchini Sudan kwamba, hali aliyoikuta nchini humu ni mbaya na kwamba Sudan inakabiliwa na wimbi kubwa la wakimbizi watoto kuliko sehemu nyinginezo zote duniani.

Katika sehemu moja ya mahojiano hayo, Elder amesema: "Tunazungumzia wasichana na wavulana 10,000 wanaolazimika kukimbia maeneo yao kila siku."

Aidha amesisitiza kwamba watoto milioni tano wanateseka kwa sababu ya vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi huko Sudan kwa karibu siku 500 sasa. Watoto wanaokimbia makazi yao mara nyingi huishia kwenye kambi ambazo hazina maji safi ya kunywa, vifaa vya matibabu wala usafi wa mazingira.

Msemaji huyo wa UNICEF vile vile ameripoti kuweko uhaba mkubwa wa chakula kote nchini Sudan na kusema kuwa sababu yake kuu ni pande zinazopigana ambazo mara kwa mara huzuia kufika misaada kwa walengwa. 

Elder ametoa mwito wa kuanzishwa upya mazungumzo kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na ameitaka jumuiya ya kimataifa kuuzingatia sana mgogoro wa Sudan.

Aidha amesema: "Mashirika ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na UNICEF, yanatatizika kuwafikia wale wanaohitaji kutokana na uhaba wa fedha, vikwazo vya urasimu, na mashambulizi yanayoendelea," na kusisitiza kuwa, mikoa 13 nchini Sudan iko kwenye ukingo wa janga la njaa na inahitaji msaada wa haraka wa kuokoa maisha.