Wanafunzi 20 wa vyuo vikuu watekwa nyara nchini Nigeria
Wanafunzi wapatao 20 wa vyuo vikuu vya Nigeria wametekwa na watu wenye silaha waliovizia magari yao kaskazini mwa nchi hiyo.
Msemaji wa jeshi la polisi katika eneo la Benue Catherine Anene amesema kwamba wanafunzi hao walikuwa wakielekea kusini mwa nchi kushiriki mkutano wa wanafunzi wanaosomea kozi ya udaktari wakati walipovamiwa katika jimbo la Benue Alkhamisi jioni.
Amesema shambulizi hilo lilitokea kando ya barabara ya Benue's Otukpo, mahali palipojulikana sana kwa utekaji nyara.
Wanafunzi waliotekwa ni wa vyuo vikuu vya Maiduguri na Jos, vyote vya kaskazini mwa Nigeria na tayari wanafunzi wenzao wamelaani tukio hilo na kuzitaka mamlaka kuwalinda wanafunzi na kuhakikisha wenzao wanaachiliwa.
Haikubainika mara moja ni kundi gani lililofanya shambulizi hilo au mahali ambapo mateka walipelekwa na polisi bado ilikuwa haijasema chochote kuhusiana na juhudi za kuwaokoa.
Kiongozi wa wanafunzi wa chuo kikuu cha Maiduguri Ijaban Bajam amesema kwenye taarifa yake kwamba wamesikitishwa na kitendo hicho na kutoa wito wa wanafunzi hao kurudi salama.
Kundi la kigaidi la Boko Haram na makundi mengine ya wabeba silaha yamekuwa yakijihusisha na utekaji nyara wanafunzi nchini Nigeria na kudai kikomboleo.
Hadi sasa wanafunzi wasiopungua 1500 wametekwa nyara huko Nigeria tangu mwaka 2014; huku makundi yenye silaha yakistafidi na mbinu hiyo ya utekaji nyara kama njia ya kupata fedha kwa ajili ya kufadhili jinai zao nyingine na kudhibiti vijiji katika maeneo tajiri kwa madini ya kaskazini magharibi mwa Nigeria hata hivyo yenye ulinzi dhaifu wa polisi.