Watu 80 wauawa nchini Sudan katika shambulio la kikosi cha RSF
Kwa akali watu 80 wameuawa kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na kikosi cha Usaidizi wa Haraka RSF katika kijiji cha kusini mashariki mwa nchi hiyo. Hayo yameelezwa na chanzo kimoja nchini humo.
Chanzo katika kituo cha matibabu cha Jalgini kimeziambia duru za habari kwamba, siku ya Alkhamisi walipokea miili 55 na makumi ya wengine waliojeruhiwa.
Chanzo hicho kimeongeza kuwa watu 25 wengine walifariki jana na na kufikisha idadi jumla ya waliopoteza maisha kufikia watu 80.
Mmoja wa manusura ameviambia vyombo vya habari kwamba, vikosi vya RSF ndio vilivyohusika na hujuma hiyo.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, mazungumzo yaliyofadhiliwa na Marekani yanayolenga kuvimaliza vita vya miezi 16 kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha RSF yanaendelea mjini Geneva Uswisi.
Sudan imekumbwa na vita kati ya jeshi, linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye ni mkuu wa Baraza la Mpito la Utawala, na kundi la RSF linaloongozwa na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo.
Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, takriban watu 12,260 wameuawa na zaidi ya 33,000 kujeruhiwa katika vita vilivyoanza Aprili 2023,
Mgogoro wa kibinadamu unaendelea kuwa mbaya zaidi kwani karibu watu milioni 6.8 wamekimbia makazi yao kutafuta usalama nchini Sudan au nchi jirani. Jitihada za kieneo na kimataifa hadi sasa ziimeshindwa kukomesha mapigano hayo.